Habari za Punde

NAIBU WAZIRI AKABIDHI MKOPO WA SH. MIL 215 KWA VIKUNDI 32 RUNGWE

Na Mwandishi wetu RUNGWE 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoa elimu ya kutosha kwa vikundi vinavyonufaika na mikopo ya kuwawezesha kiuchumi ili viweze kujikwamua.

Mhe. Mwanaidi  akikabidhi mkopo wa sh 215 kwa vikundi 32 vya Halmashauri ya Wilaya Rungwe amesema vikundi hivyo vikipata elimu vitasaidia kuleta Maendeleo ya kiuchumi kwa wao wenyewe na Taifa.

"Tusisite kuwapa mikopo wananchi wanaojitolea kujiunga katika vikundi tuwape elimu ya kutosha kadiri ya mipango yao na mahitaji yao ili waweze kujiendeleza na kuhakikisha hawakwami katika mipango yao na wanasonga mbele" alisema Mhe. Mwanaidi.

Mhe. Mwanaidi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe kwa kusimamia vizuri mapato na kutenga fedha za mkopo kuwawezesha wananchi na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kujiunga vikundi ili wanufaike na mikopo hiyo.

Awali akiwasilisha taarifa ya mikopo hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe alisema katika fedha hiyo, sh. milioni 60 ni kutokana na mapato ya ndani na sh. milioni 155 ni sehemu ya fedha za marejesho ya mikopo.

Aidha, Mchau Ameongeza kuwa Halmashauri kwa kushirikiana na Wadau wamekuwa wakitoa mafunzo kwa vikundi hivyo ili kuhakikisha mikopo inatumika ipasavyo na kurejesha kwa wakati ili wananchi wengine wanufaike.

Mchau amesema kwa robo ijayo ya mwaka, vikundi vitakavyopewa kipaumbele kwenye mikopo ni vile vitakavyokuwa na mweleko wa kuwa na viwanda na kutoa ajira kwa wengine ikiwemo kikundi Cha "Bamboo" kinachotarajiwa kuanza uzalishaji wa vijiti vya kusafishia meno (toothpick) kilichopo kata ya Isongolo Wilayani hapo.

"Kwenye mfuko wetu wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu tuna jumla ya sh. milioni 1.8 zipo katika mzunguko, tulishakaa na kukubaliana kuwa ifikie hatua tuwe na vikundi vya Wanawake na vijana vyenye kuleta tija kwa kuwa kampuni, vinavyoweza kukopesheka kwenye benki lakini pia kutoa ajira na kusaidia katika uchumi wetu" 

Kwa upande wao baadhi ya wanavikundi waliopata mkopo huo wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuhakikisha wanawainua kiuchumi kwani mikopo hiyo inawasaidia kuongeza mitaji ya shughuli zao hivyo kuongeza uzalishaji na kuweza kutunza familia zao.

"Kikundi chetu kina ng'ombe wa maziwa na tuna uwezo wa kutoa Lita 47 kwa siku, leo hii tumepata mkopo mkubwa sh. mil 22 tunategemea kuongeza ng'ombe zaidi na hapo baadaye tunatarajia kuwa na kiwanda cha kusindika maziwa na kuajiri vijana wengi" amesema Kaimu Juma mmoja wa wanufaika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.