Habari za Punde

Uzinduzi wa Muongozo wa Kushughulikia Mwili na Mazoezi ya Viungo Kuimarisha Afya. “Tuache Tabia Bwete Tupunguze Maradhi Yasioambukiza”

Na.Kassim Abdi.OMPR Zanzibar.                                                                                       

Wananchi wametakiwa kutenga muda maalum wa kufanya mazoezi ili kupunguza          ongezeko la magonjwa  yasiyoambukiza.                                                                          

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alitoa wito katika hafla ya uzinduzi wa muongozo wa kuushughulisha mwili na mazoezi ya viungo ili kuimarisha afya, iliyofanyika katika Hotel ya Verde Mtoni.

Alisema kukosekana kwa muda wa kufanya mazoezi kunasababisha kuongezeka kwa maradhi mbali mbali ikiwemo  kiharusi, mafigo kushindwa kufanyakazi na kupoteza viungo kutokana na ugonjwa wa kisukari pamoja na magonjwa mengine.

Alieleza muongozo huo umetoa maelekezo ya kufanya mazoezi kwa makundi ya rika zote wakiwemo wazee, Vijana,wajawazito, watu wenye ulemavu, pamoja na kugusia suala la matumizi ya lishe bora kwa mlo uliokamilika na kujiepusha na kubweteka.

Mhe. Hemed alisema Serikali imechukua hatua mbali mbali ikiwemo kutoa elimu ya afya na imeongeza vituo vya afya kutoka vinane (8) hadi khamsini na tatu (53), hivyo aliwakumbusha wananchi kuwa na tabia ya kufika  katika vituo hivyo kwa ajili ya kujua afya zao.

Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa wizara ya afya na taasisi zinazohusika na michezo kusimamia muongozo huo  kupitia viongozi wa vikundi vya mazoezi na makundi mbali mbali ili wananchi waweze kufaidika vyema na muongozo huo.

Aidha, aliomba skuli zote za msingi na sekondari pamoja na vyuo vikuu viandae na kuendelea kusimamia muda wa kuushughulisha mwili na kufanya mazoezi kwa wanafunzi ili kukuza afya zao kwa kufahamu kuwa afya imara huongeza ufahamu.

Nae Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii, wazee,Jinsia na Watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazrui alieleza kuwa muongozo huo utasaidia wananchi kujua aina ya mazoezi wanayotakiwa kufanya kwa mujibu wa mahitaji ya hali za Afya zao.

Aliishauri Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kujenga maeneo ya michezo katika nyumba za maendeleo zinazoendelea kujengwa nchini ili kutoa fursa kwa wananchi kutumia maeneo hayo kuushugulisha mwili na mazoezi.

Akisoma risala Dk. Lulu Omar alieleza kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliopita kumekuwa na ongezeko la idadi ya watanzania kupata magonjwa yasiyoambukiza ambapo hadi kufikia mwaka 2020 wagonjwa wamefikia milioni 4.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 41% ya wagonjwa hao.

 Alieleza kuwa, kwa mujibu wa takwimu za Shirika la afya ulimwenguni za mwaka 2008 zinaonesha magonjwa hayo yanachangia vifo zaidi ya milioni 41 kwa mwaka ambayo sawa na asilimia 71% ya vifo vyote vinavyotokea ulimwenguni.

Akitoa salamu za Shirika la Afya Duniani (WHO) muwakilishi wa shirika hilo Dk. Ghirmay Andemichael alisema maradhi yasiyoambukiza hupelekea kupunguza nguvu kazi ya taifa kwa kusababisha watu kukosa uwezo wa kushiriki katika shughuli za kimaendeleo na kupelekea kuathiri hali ya kiafya, kiuchumi na kijamii.

Katika kutatua changamoto hiyo aliwashauri wananchi kuwa na kawaida ya kufanya mazoezi ili kuchangamsha mwili na kuuweka katika hali ya imara Zaidi jambo litakalosaidia kuepukana na maradhi yasioambukiza.

Kauli mbiu ya uzinduzi huo inasema “TUACHE TABIA BWETE TUPUNGUZE MARADHI YASIOAMBUKIZA”

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.