Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza
haja ya wananchi kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, kwa kigezo kuwa ndio
msingi wa maendeleo ya nchi.
Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo, wakati alipojumuika pamoja na waumini wa Dini ya Kiislamu katika sala ya Ijumaa iliofanyika Masjid Fatma, Kibanda Hatari kwa Sheikh Mohamed Ali, Jijini Zanzibar.
Amesema ili Taifa liweze kupata maendeleo, kuna umuhimu mkubwa wa jamii kudumisha amani, umoja na mshikamano uliopo.
Aidha, amewakumbusha Viongozi na watendaji umuhimu wa kuwajibika katika maeneo yao ya kazi, kila mmoja kwa nafasi yake, sambamba na kutilia mkazo suala zima la uadilifu katika maeneo ya kazi, ikiwemo utoaji wa huduma za jamii kwa wananchi.
Mapema Khatibu wa Sala hiyo ya Ijumaa, Sheikh Omar Abdi aliwataka waumini kushikamana na kuendelea kuitunza amani na utulivu uliopo nchini unaotokana na juhudi za Viongozi za kuwaunganisha wananchi.
Aidha, amesema wananchi wana jukumu kubwa la kuwatii viongozi walioko madarakani sambamba na kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao na kuwa waadilifu ili nchi iendelee kupata neema.
Kitengo cha habari,
Ikulu Zanzibar
No comments:
Post a Comment