Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi Amefungua Msikiti wa Masjid Al Noor Unguja Ukuu Kaepwani Wilaya ya Kati Unguja leo 26-11-2021.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wananchi wa Kijiji cha Unguja Ukuu Kaepwani Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa na hafla ya ufunguzi wa Masikiti wa Masjid Al Noor Unguja Ukuu Kaepwani, baada ya kukamilika kwa ujenzi wake

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka waumin wa Dini ya Kiislamu Shehiya ya Unguja Ukuu, kutumia vyema msikiti wa Al-Noor kwa ajili ya kujadili matatizo yanayoihusu jamii na kuyatafutia ufumbuzi.

Alhaj Dk. Mwinyi ametoa ukumbusho huo kwa waumini wa Dini ya Kiislamu wa Shehiya ya Unguja Ukuu na Vitongoji vya jirani wakati alipozungumza nao katika hafla  ya ufunguzi wa  Msikiti wa Ijumaa  (Masjid Al-Noor) baada ya kukamilika ujenzi wake, tukio lililokwenda sambamba na Ibada ya sala ya Ijumaa.

Amesema kuna umuhimu kwa waumini hao kutumia vikao vya msikiti na kujadili masuala mbali mbali pamoja na changamoto zinazoihusu jamii, wakiwemo mayatima, wajane pamoja na walemavu na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili.

Aliwaeleza  waumini hao, kama walivyofanikiwa kuanza kwa mafanikio ujenzi wa msikiti huo na kufikia  hatua ya kuridhisha , ndivyo wanavyoweza  kukaa pamoja na kujadili changamoto na maovu yanayoihusu jamii, ikiwemo suala la udhalilishaji ambalo limeshamiri.

Alieleza kuwa mapambano dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia ni jambo linalohitaji nguvu ya jamii na sio suala linaloihusu Serikali pekee.

Aidha, alisema kuwepo umuhimu mkubwa kwa jamii hiyo kutafuta njia za kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya, tatizo linalohusisha kundi kubwa la vijana.  

Alhaj Dk. Mwinyi aliwashukuru waumini wote waliosaidia na kutoa michango yao kufanikisha ujenzi wa msikiti pamoja na wafadhili mbali mbali.

Sambamba na hilo, akaitaka kamati ya msikiti huo kusimamia michango ya waumini ili waweze kuutunza msikiti huo  na kubaki katika hali ya unadhifu, kuwatunza wanaousimamia pamoja na walimu wa madrasa wanaofundisha dini wanafunzi.

Mapema, Naibu Kadhi Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahamoud Mussa Wadi aliwataka waumini hao kuepuka mifarakano, kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza  pamoja na kudumisha usafi  wa masikiti.

Aidha, Sheikh Khalid Ali Mfaume, akatoa salamu za Ofisi ya Mufti  na kusema Rais wa Zanzibar na Mwenyekitii wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi  ana nia njema na wananchi wake, kwani maeneo mbali mbali aliyopata fursa ya kuyatembelea yameweza kunufaika kutokana na utekelezaji wa ahadi alizoweka katika kusaidia maendeleo ya misikiti,uislamu pamoja na maendeleo kwa ujumla.

Nae, Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Hadidi Rashid Hadidi aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Alhad Dk. Mwinyi kwa wito wake wa mara kwa mara wa kuitaka jamii kudumisha amani na utulivu, hatua iliyoa fursa ya kufanya Ibada kiasi ambacho misikiti miwili mikubwa imefunguliwa Mkoani humo katika kipindi cha mwaka mmoja wa Uongozi wake.

Mkuu huyo wa Mkoa aliahidi kusimamia taratibu zote za uwekaji wa Tuta katika neo la Msikiti Al-Noor, baada ya wananchi kuomba kujengewa tuta hilo ili kuwaepusha waenda kwa miguu, ikiwemo watoto  na hatari ya kugongwa na magari.

Katika sala hiyo ya Ijumaa iliosalishwa na Sheikh Suleiman Feisal Al-Kindi, Khatibu wa Sala hiyo Sheikh Othman Maalim alimuiomba Mwenyezi Mungu awabariki waislamu wote waliochangia ujenzi wa msikiti huo, sambamba na kutoa wito wa kutumika vyema msikiti huo katika  kuimarisha uislamu na kufanya kuwa mahala pa salama.

Msikiti wa Al-Noor unaohusisha na eneo la Madrasa una uwezo wa kuswaliwa na waumini wa kike na kiume ambapo ujenzi wake ulianza  mnamo mwaka 2006 na kupita katika hatua mbali mbali hadi kukamilika kwake.

Ukamilishaji wa msikiti huo umetokana na maombi ya waumini wa msikiti huo ambao walimuomba Alhaj Dk. Mwinyi mnamo Juni 18, 2021 wakati alipokwenda kuungana nao na kusali pamoja sala ya Ijumaa na ndipo Rais alilipokea ombi hilo na mnamo mwezi Agosti ujenzi ulianza.                                                                                

Imetayarishwa na

Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.