Chama cha Waandishi wa Wahabari Wanawake Tanzania, Zanzibar, (TAMWA ZNZ) kinawapongeza Bi Salma Ali Hassan Khamis na Bi Mwanamkaa Abdulrahman Mohammed kwa kuteuliwa kuiongoza Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.
Afisi
ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar ina majukumu mengi yakiwemo ya kupokea na kukagua faili zote zinazotoka
polisi, kuchambua ushahidi wa upelelezi uliotoka polisi, kupeleka faili za kesi
mahakamani, kuendesha kesi Mahakamani kwa kuuwakilisha upande wa Serikali na
kukata rufaa iwapo haitaridhika na maamuzi ya Mahakama kuhusiana na shauri
lolote
Kupitia
uteuzi huo uiliofanywa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar,Dkt Hussein Ali Mwinyi hivi karibuni, Bi Salma
Ali Hassan Khamis ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Afisi hiyo na Bi Mwanamkaa
Abdulrahman Mohammed kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka katika Afisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar.
Hawa
ni viongozi wa kwanza wanawake kuongoza Afisi hiyo katika nafasi hizo kuu
kabisa na hivyo kuongeza uwepo wa wanawake katika nafasi za uongozi kwa jumla,
hali ambayo inahimizwa kwa maendeleo ya mwanamke na nchi kwa jumla.
TAMWA
- ZNZ inaamini kuwa kuwepo kwa viongozi hao, kesi za udhalilishaji na ukatili
wa wanawake na watoto zitapata msukumo mpya katika ufuatiliaji na uchunguzi na
kwa muda mfupi ili kukomesha kabisa vitendo hivyo vilivyokithiri nchini na
ambavyo vinawaathiri zaidi wanawake na
watoto.
Kwa
mujibu wa takwimu kutoka Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, jumla ya kesi 838 za udhalilishaji ziliripotiwa kuanzia
mwezi wa Januari hadi Agosti, 2021 ambapo wanawake walioathirika ni 679 sawa na
asilimia 81 na wanaume ni 166 sawa na asilimia
19.8.
Ukatili
mwingine ni wanawake na watoto kupigwa kwa mapanga kutokana na sababu
zisizokuwa za msingi na kwamba wengi wa wahalifu bado hawajakamatwa. Hivyo,
tunashauri Wakurugenzi wa Mashtaka kuandaa
utaratibu maalum wa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kurahisisha uchunguzi
katika matukio ya aina hii.
TAMWA
- ZNZ inawatakia kila la kheri Wakurugenzi hao katika majukumu yao mapya na muhimu na Mwenyezi
Mungu awaongeze hekima, busara, ushirikishaji na uadilifu zaidi.
Dk. Mzuri Issa
Mkurugenzi
TAMWA, ZNZ
No comments:
Post a Comment