Habari za Punde

Mkoa wa Tanga Waweka Misingi Bora ili Kufufua Kilimo cha Korosho.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

SERIKALI mkoani Tanga inaendelea kujenga misingi ya kurejesha zao la korosho kama zao kubwa na tegemezi kwa wananchi wa Mkoa huo ambalo pia litachangia kwenye kipato na kuwaondolea umasikini.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima ofisini kwake wakati akiongea na uongozi wa Bodi ya Korosho na kusema katika Mkoa kuna Wilaya tatu ambazo zipo kipaumbele katika kilimo cha zao hilo.

"Tunaangalia kwenye msisitizo mkubwa ambapo ni Wilaya za Pangani, Mkinga lakini pia kwenye Wilaya za nyongeza ambazo zinaweza zikaingia kwenye mchakato huo na kuongeza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa korosho katika Mkoa wetu ni Wilaya ya Muheza ambayo iko katikati pale ambayo nayo ina asili ya korosho kwa muda mrefu lakini pia Wilaya za Korogwe na Handeni" alifafanua.

Aidha Malima aliongelea kuhusu kupata masoko ya ndani ya Mkoa kwa wakulima wa korosho kutokana na wakulima hao kupeleka mazao yao katika masoko ya jirani, ambapo misingi inatakiwa kuwekwa vizuri ili wakulima waweze kuuzia mazao yao ndani ya Mkoa.

"Tukiweka misingi mizuri ya soko ambapo mkulima anapata bei nzuri akiwa hapahapa, hana haja ya kuvusha korosho yake kuipeleka nje ya Tanga, na kwa maana hiyo badala ya kupata sh 1000 kwa kilo moja, akipata hiyohiyo sh 2000 hadi 2100 ambayo ndiyo bei ya mnadani inayotoka mkoani Lindi, akiipata hapahapa Tanga hakuna mtu atatorosha korosho zake" alisema.

Malima alieleza kwamba kuna ubovu wa kutunza mashamba lakini wao Mkoa watalisimamia hilo na kwenda kuhamasisha uzalishaji wa zao hilo  huku wakikubaliana na Bodi kuealetea pembejeo kwa wakati pamoja na wataalamu watakotoa elimu jwa wakulima jinsi ya kulima kilimo bora.

"Kuna ubovu wa kutunza mashamba, korosho siri yake ni kutunza mashamba, kupalilia na kupiga dawa kwa wakati, suala la dawa ni la Bodi lakini suala la kupalilia na nidhamu ya kutunza mashamba ni la mkuu wa Mkoa, kwahiyo tumekubaliana hapa na Bodi kwamba sisi tunakwenda kuhamasisha uzalishaji wa zao la korosho ili tutoke kwenye tani 2500 na kufikia tani 4500" aliongeza mkuu huyo.

Vilevile alibainisha kwamba ndani ya halmashauri mbili za Wilaya za Pangani na Mkinga zinaweza kunufaisha Mkoa pekee kwa kilimo hicho bila kutegemea mazao ya samaki na matunda ambavyo pia huingiza pato la Taifa kupitia halmashauri hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo nchini Brigedia mstaafu Aloyce Mwanjile alisema Bodi imeonekea Mkoa wa Tanga uko kiuzalishaji na kuna maeneo ambayo yanaweza kuzalisha korosho kwa wingi lakini pia wamekubaliana na mkuu wa Mkoa kuufijia Mkoa huo ili kuinua kilimo hicho.

"Tumeona Tanga kama ndio Mkoa ambao una nafasi kubwa ya kuzalisha zao la korosho, hivyo tumekuja na kutembelea maeneo mbalimbali hari Wilaya ya Mkinga ambayo inaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuzalisha korosho na baada ya ziara yetu sasa tumepata nafasi ya kujadiliana na mkuu wa Mkoa" alisema.

"Mkuu wa Mkoa ametuahidi kwamba yuko tayari kuhakikisha uzalishaji unaingezeka, sisi pia kama Bodi tumemuahidi kwamba tuko tayari kutoa msaada, kwa maana ya kutoa viuatilifu, mbegu kwa wakati lakini pia kuhakikisha kwa kushirikiana na kituo cha utafiti cha TARI Naliendele kuwaleta wataalamu kwa ajili ya kutoa elimu" aliongeza 

Hata hivyo Brigedia Mwanjile alisisitiza kwamba "tija ya zao hili unaingezeka kwa Mkoa huu wa Tanga na hivyo kuwezesha pia kuondoa umasikini kwa wananchi wetu, kama ilani ya Ccm inavyohitaji" alieleza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.