Habari za Punde

Wafanyabiashara 350 kushiriki Tamasha la Biashara Zanzibar

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaabani akizungumza na waandishi wa habari Kuhusu tamasha la nane la Biashara ambalo litaanza Januari 2 Hadi Januari 15  katika Viwanja vya Maisara Wilaya ya Mjini , ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kusherehekea miaka 58 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar,hafla hiyo ilifanyika Ofisi za Wizara ya Biashara Malindi

                  Picha na Fauzia Mussa -- Maelezo Zanzibar.

Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar . 28/12/2021.

Kiasi ya Wafanyabiashara 350  kutoka nchi mbali mbali wanatarajiwa kushiriki Tamasha la biashara la Zanzibar  linalotarajiwa kuanza Januari 02 hadi Januar 15 mwaka 2O22 katika viwanja vya Maisara Wilaya ya Mjini . .

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaaban ameyasema hayo  wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Malindi .

Amesema tamasha hilo litatoa fursa za kibiashara, kuongeza ujuzi na wigo kwa wajasiriamali wadogo wadogo wenye viwanda pamoja na Taasisi za Serikali zinazotoa huduma mbali mbali kwa jamii.

Alisema ni miaka minane  tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo, kupitia Wizara ya Biashara ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra ya maadhimisho ya miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar .

Nchi zinazotarajiwa kushiriki katika tamasha hilo ni pamoja na Uganda,Kenya, Misri, Burundi , Tanzania bara na wenyeji Zanzibar ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni Teknolojia na Ubunifu katika ukuaji wa Biashara .

lengo ni kukuza biashara kwa kutumia teknolojia ya kuuza na kununua bidhaa kwa njia ya mtandao na wajasiriamali wachanga kutumika na kuengezeka thamani .

Hata hivyo aliwataka Wananchi kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la nane la biashara la Zanzibar kwa  kununua bidhaa zenye ubora za ndani na nje ya nchi .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.