Habari za Punde

Watakwimu Nchini Watakiwa Kufanyakazi kwa Weledi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akitoa hutuba wakati wa mahafali ya saba ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika ambapo aliwataka Watakwimu hao kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha uandaaji wa takwimu unakidhi ubora na mahitaji ya kitaifa na kimataifa jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akimtunuku cheti mwanafunzi aliyemaliza elimu yake wakati wa mahafali ya saba ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrik ya.liyofanyika jijini Dar es Salaam
Baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni ( hayupo pichani) wakati wa hafla ya mahafali ya saba ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika katika hafla ya mahafali ya saba ya chuo  hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

(Picha na WFM Dar es Salaam)

Na Josephine Majura WFM, Dar es Salaam.

Watakwimu nchini watakiwa kufanya kazi kwa weledi na kwa viwango vya kimataifa ili kuhakikisha uandaaji wa takwimu unakidhi ubora na mahitaji ya kitaifa na kimataifa hususan katika Dira ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2030. 

 

Wito huo ametolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), wakati wa mahafali ya saba ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, yaliyofanyika jijini Dar es salaam.

 

“Natambua mchango muhimu wa Sekta ya Takwimu rasmi katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 na malengo ya maendeleo ya Kikanda na Kimataifa”, alisema Mhandisi Masauni.

 

“Tusisahau kuweka jitihada maalum katika Sayansi ya Data ili kuendana na kasi ya mahitaji ya watumiaji wa takwimu na mabadilko ya kiteknolojia”, alisisitiza Mhandisi Masauni.

 

Aliongeza kuwa mnamo mwezi Septemba, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alizindua Kitabu cha Mkakati wa Uelimishaji na Uhamasishaji wa Zoezi la Sensa kama ishara ya uzinduzi rasmi wa zoezi muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.

 

Mhandisi Masauni, alisema kuwa zoezi la uelimishaji na uhamasishaji liendelee kutolewa  kwa kuwa ni muhimu katika kupata taarifa za watu na makazi, mahali wanapoishi, uhamaji kati ya vijijini na mijini, idadi ya wakazi, jinsi, umri, ulemavu, shughuli za kiuchumi na kadhalika ili kupima maendeleo tangu sensa ya mwisho iliyofanyika mwaka 2012hatua itakayochangia mgawanyo mzuri wa rasilimali za maendeleo katika nyanja za afya, elimu, maji na nishati.

 

Alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imetoa fedha kwa ajili ya kusomesha Wahadhiri katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu, hivyo ni jukumu la wasomi kuelekeza jitihada za kiutafiti katika Mapinduzi ya Takwimu ili kujenga uwezo wa kutathmini Dira ya Maendeleo ya Taifa inayoisha mwaka 2025 pia Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu yatakayoisha mwaka 2030.

 

Aidha, Mhandisi Masauni aliwashukuru Wadau wa Maendeleo hususan Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao mwaka huu wamechangia vifaa vya kufundishia katika chuo hicho na Benki ya Dunia (WB) ambao wametoa fedha za maboresho mengine makubwa katika Sekta ya elimu ya juu nchini ambapo Chuo pia kimenufaika kupitia Mpango huo.

 

Pia aliwashukuru Kamisheni ya Uchumi Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA), Waheshimiwa Mabalozi, Maofisa Wakazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Washirika wa Maendeleo; na Wakurugenzi Wakuu wa Ofisi za Taifa za Takwimu za Nchi Wanachama wa Chuo.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kanda ya Ushauri ya Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, ambae ni Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa, alimhakikishia Mhandisi Masauni kwamba wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika mwakani, Watakwimu wataendelea kufanya kazi kwa weledi kwa kuwa sensa ni muhimu kwa Serikali katika kupanga maendeleo.

 

Naye Mkuu wa Chuo cha cha Takwimu Mashariki mwa Afrika, Dkt. Tumaini Katunzi alisema kuwa katika kuhakikisha Chuo kinaendana na soko la ajira duniani katika mwaka wa masomo 2021/2022 wamedahili wanafunzi katika programu mpya ambazo ni Shahada ya Sayansi ya Data na Shahada ya Uchumi na Takwimu za Biashara.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb) amewatumuku jumla ya wahitimu 147 wakiwemo wanawake 56 na wanaume 91 na kati ya hao wahitimu 146 na Mmoja kutoka nchini Somalia. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.