WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kuwekeza hapa nchini dola za Marekani bilioni 2.47 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Nyanja za kiuchumi na kijamii.
Dkt. Nchemba ametoa shukrani hizo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Kipronoh Cheptoo, anayesimamia nchi nane za kiafrika katika Benki hiyo, ambazo ni Tanzania, Kenya, Ethiopia, Rwanda, Seychelles, Sudan Kusini, Eritrea na Uganda.
Alisema kuwa Benki hiyo imeipatia Tanzania mikopo nafuu na misaada kwenye miradi 23 ya maendeleo ambapo asilimia 87 ya miradi hiyo iko katika sekta ya miundombinu ikiwemo nishati, barabara, maji na usafi wa mazingira na asilimia 13 imeelekezwa kwenye sekta za kilimo, sekta binafsi na utawala wa kiuchumi.
“Kwa niaba ya Serikali na Wananchi, ninapongeza uungaji mkono wa Benki ya Maendeleo ya Afrika katika maendeleo ya nchi kwa kuwa miradi hiyo mikubwa inayotekelezwa kupitia fedha zinazotolewa na Benki hiyo zimesaidia kukuza uchumi wa nchi ikiwemo miradi ya barabara ya Ukanda wa Mtwara, Katavi na Tabora” alisema Dkt. Nchemba.
Aliitaja miradi mingine inayofadhiliwa na AfDB kuwa ni Kituo cha Pamoja cha Forodha katika Mpaka wa Kenya na Tanzania-Namanga, ambao umesaidia kukuza biashara kati ya nchi hizo mbili pamoja na Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira-Arusha, ambao umeboresha maisha ya wananchi wa mkoa huo.
Dkt. Nchemba aliitaja miradi mingine muhimu ambayo Benki ya Maendeleo ya Afrika imetoa fedha ikiwa ni pamoja na Mradi wa Barabara za Mzunguko katika Jiji la Dodoma ambazo alisema zitafungua fursa za kiuchumi wa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani pamoja na Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bw. Kipronoh Cheptoo, aliipongeza Tanzania kwa umahili wake wa kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayochangia ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.
Aliahidi kuwa Benki yake iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania ambayo ni mshirika ama mwanachama wa Benki hiyo, kwa kutoa fedha zaidi zitakazosaidia kukamilisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Bw. Cheptoo alisema kuwa AfDB itatoa fedha pia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mipya inayohusu sekta tatu ikiwemo program ya kuendeleza mapinduzi ya viwanda katika kilimo, uendelezaji wa stadi za kazi na ajira kwa vijana pamoja na mradi wa ujenzi wa Barabara ya Ifakara-Malinyi-Londo hadi Lumecha, uliokusudiwa kuiunganisha mikoa wa Morogoro na Ruvuma kwa ajili ya kukuza fursa za sekta ya kilimo katika maeneo hayo.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ya Waziri wa Fedha na Mipango, Jijini Dodoma, yalihudhuriwa na Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia madeni, Bi. Amina Khamis Shaaban, pamoja na wakuu kadhaa wa Idara kwa upande wa Tanzania na Mshauri Mwandamizi wa masuala ya kiuchumi wa AfDB, Bw. Jonathan Nzayikorera pamoja na Kaimu Meneja wa Benki hiyo nchini Tanzania, Dkt. Jacob Oduor.
No comments:
Post a Comment