Habari za Punde

PEMBE YA WASUMBWA ILIYOWAMALIZA WAGOGO

 
Na.Adeladius Makwega. Dodoma.

Watu wengi ambao kidogo waliwahi kusoma historia ya makabila mara zote wanatambua kuwa kabila la Wasumbwa huwa ni sehemu ya kabila ya Wanyamwezi. Lakini wapo Watanzania wengi wa leo ambao wanazaliwa na wazazi wanaotokea eneo ambalo kwa asili ni la Wasumbwa hudhani kuwa wao ni Wanyamwezi kumbe ni Wasumbwa.

Inaaminika kuwa Wasumbwa wengi wapo katika sehemu ambayo leo hii Kijiografia ni Wilaya ya Kahama.

Kwa kuwa Tanzania ni kubwa, naamini wapo watu ambao hawana asili ya Unyamwezi wala Usumbwa ambao katika maisha yao walishawahi kutembelea maeneo ambayo kabila la Wasumbwa wapo na walipofika huko walipachikwa jina la “BANAMAHANGA”au “BANAMINKO”. Neno Banamahanga ni neno linalotoa ishara kwa watu wageni wanaotembelea makaazi ya Wasumbwa. Nalo neno Banaminko linamanisha kuwa mtu huyu hana mahusiano kabisa na Wasumbwa. Maneno hayo mawili hayamanishi utani bali huwatambulisha watu waliowageni na Wasumbwa tu.

BWIMEZI/ BIMENZI ni neno linalomaanisha utani na kabila la Wasumbwa ambao kama yalivyo makabila mengine utani huo unaweza kuwa katika ngazi ya familia, ngazi za ukoo na ukoo na hata kwa makabila mengine.

Wasumbwa wakati na kabla ya biashara ya utumwa na ujio wa Waarabu walikuwa wakifanya biashara ya kusafirisha baadhi ya bidhaa kutoka Kongo hadi Bagamoyo, ambapo huko Wasumbwa walibadilishana na shanga, bunduki na nguo. Wasumbwa walielewana mno na Wazaramo kwa kuwa walipofika Pwani, Wasumbwa walipata pia nyumba za konokono ambazo huko bara zilitumika kama fedha na mapambo kwa machifu wa Wasumbwa walizovaa shingoni, zikifahamika kama “Nsimbi ne vilungu vya bami.”

Wazaramo waliwatania Wasumbwa wakisema kuwa watakufa kwa utafutaji wa utajiri huo kutoka kwao hadi Pwani. Wazaramo waliwaambia Wasumbwa kuwa ni wapagazi wa mizigo ya Waarabu kama walivyo Wanyamwezi. Utani ulikuwa mkubwa na hata Wasumbwa walipokuwa safarini kutoka kwao kwenda pwani wengine walifariki wakiwa Pwani, Wazaramo walichukua jukumu la kuwazika katika ardhi yao.

Mara baada ya maziko Wasumbwa walipopita tena, Wazaramo waliwaambia kuwa ndugu yenu kafa na kaburi lake lipo pale, Wasumbwa walitambua kuwa huo ni utani na si kweli wakati kumbe lililokuwa linasemwa na Wazaramo lilikuwa la kweli.

Wasumbwa nao walipokuwa wakikutana na Wazaramo wakichimba kaburi kuzika ndugu zao waliofariki, Wasumbwa waliwacheka mno Wazaramo, nakuwaambia kuwa “Mlamalile hansi.” Wakimaanisha kuwa mtamalizika wote kuzikwa ardhini.

Kabila lingine ambalo lina utani na Wasumbwa huwa ni Wagogo, kama nilivyokudokeza kuwa Wasumbwa walikuwa wakifanya biashara tokea Kongo kwenda Bagamoyo kwa hiyo Dodoma ilikuwa ni njia yao kuu ya kupita. Wagogo walikuwa mabingwa wa kutengeneza viatu kwa kutumia ngozi za wanyama. Kwa hiyo Wasumbwa walikuwa pia wakinunua viatu vya Wagogo safarini.

Wagogo walitumia mbinu za kivita kuwavamia Wasumbwa wakati wanapotoka Bagamoyo kwani walikuwa na bunduki, shanga na nguo. Wagogo walitambua kuwa Wasumbwa wana vitu walivyovipata kutoka huko, hapo ndipo Wasumbwa walishambuliwa ipasavyo na kupokonya mali zote.

Kuna wakati Chifu wa Wasumbwa aliyefahamika kama Kafuku alipita Ugogoni na kwenda Bagamoyo alipofika huko alifungasha vitu vyake kadhaa na msafara wake na kurudi kupitia njia aliyokuja nayo kurejea Kahama, akiwa na msafara wake mkubwa, Wagogo waliuvamia msafara huo na kuwapokonya vitu vyote na kibaya zaidi walimuuwa Chifu wa Wasumbwa Kafuku.

Kama ilivyo tukio lolote la uvamizi, baadhi ya waliokuwepo katika kundi la msafara wa Chifu Kafuku waliwaponyoka Wagogo na kurudi salama hadi Kahama. Walipofika huko walieleza tukio lililofanywa na Wagogo na namna walivyomuua Chifu Kafuku.Wasumbwa walichukizwa na tukio hilo sana sana.

Tabia ya Chifu Kafuko mara zote alipokuwa katika misafara yake kutoka Kongo hadi Bagamoyo na kurudi alikuwa akitembea na pembe ambayo ilikuwa na madawa ya asili. Kazi kubwa ya pembe hiyo ilikuwa ni kuwalinda na mvua isinyeshe wakati wa kwenda na wakati wa kurudi.

Inaaminika kuwa dawa zilizokuwa zinawekwa katika pembe hiyo zilikuwa zinatokana na mti uliyofahamika kama “Mti gwe Nsima.” Kwa kiswahili ni mti wa Nsima.

Ilikuwa ikiaminika kuwa kuwa wakati dawa hiyo inatayarishwa, mdudu yoyote wa jamii ya nzi hakuweza kusogea. Huku wakiamini kuwa kama mtu angeuchimba na kuondoa mti huo, alikuwa anakufa muda huo huo, kwa kukosa pumzi. Jirani na mti huo, mvua ilikuwa hainyeshi hata mara moja. Wakisema kuwa hata yule aliyekwenda kuchimba dawa ili awe salama alitakiwa kuwa na kuku mweupe mkononi kwa kafara.

Wagogo walivyomuuwa Chifu Kafuku ile pembe yenye dawa hizo ilianguka chini katika varangati hilo na cha kustajabisha wakati wa mchana pembe hiyo ilikuwa inalia na kutoa machozi ya damu, usiku ilikuwa inatoa miale ya moto. Jambo hilo liliwachanganya mno Wagogo. Tangu tukio hilo Wagogo walikumbwa na ukame mkubwa na mvua haikunyesha na kukaibuka njaa kubwa, Wagogo walianza kufariki.

Machifu na wazee wa Kigogo waliketi kulijadili jambo hilo na walipoenda kwa mganga ilibainika kuwa chanzo ni kuwepo kwa pembe ya Kafuku ambayo ndiyo ilikuwa inazuia mvua. Wagogo walipoambiwa hilo, mwanzoni walipinga lakini hali ilikuwa mbaya sana na jambo hilo lilifanya wafunge safari hadi nyumbani kwa Chifu Kafuku huko Mbogwe-Kahama.

Walieleza kilichotokea na uhaba wa mvua unaowakumba, walielezwa waombe msamaha kwa kumuua Chifu Kafuku na walete mifugo 300 kama adhabu kwa kosa hilo ili mvua na vifo visitokee katika jamii ya Wagogo. Ndugu wa Chifu Kafuku waliwasamehe Wagogo kwa hiyo walikubali wakatoka Kahama na kufika Dodoma wakaichukua pembe ile na kuichoma moto na wakati huo huo mvua ikanyesha na njaa ikapotea Ugogoni.

Tangu wakati huo Wasumbwa wamekuwa watani wakubwa wa Wagogo kutokana na tukio hilo. Wasumbwa wakawa wanasema “Mwabona ihembe lye mwa Kafuku Lyamala Bagogo.” Mmeona pembe ya Kafuku ilivyowamaliza Wagogo.

Mpaka leo Wasumbwa wanawaambia wagogo msilete utani na sisi, pembe tu imewatoa jasho, tutawamaliza kabisa wote.

makwadeladius@gmail.com

0717649257.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.