Habari za Punde

JE UNAWAFAHAMU WAPARE? (I)

Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Katika Lugha ya Kipare (KICHASU), wanatumia neno ITHOLA wanapomaanisha utani, wingi wa neno hilo huwa MATHOLA, linapotumika kama kitendo huwa KUTHOLA na pale watu wanapotaniana huwa KUTHOLANA.

Kabla sijaingia kwa kina katika utani huo ni vizuri msomaji wa matini haya kuwafahamu Wapare ni kabila linalopatikana katika mkoa wa Kilimanjaro tangu enzi, huku wakiwa miongoni mwa makabila ya Wachaga na Wamasai ambayo yanapatikana mkoa huo ulio jirani  na Mlima Kilimanjaro uliyo mrefu barani Afrika.

Mtani mkubwa wa Mpare ni Mchaga ikiaminika kuwa hilo linatokana na vita walivyopigana ndugu hawa wakati wa karne ya 19. Inadaiwa wakati huo wa mapambano hayo Wachaga waliwashinda Wapare vilivyo.

Wakati wapo katika uwanja wa vita Wachaga hao walikuwa wakisema kuwa MPARE MPARE MPARE ikimaanisha MPIGE MPIGE MPIGE.

Kwa hiyo neno MPARE ni la Kichaga ambalo linatokana na mapambano hayo baina ya Wachaga na Wapare vitani. Swali la kujiuliza kwanini ndugu hawa waitwe kwa kutumia lugha ya kabila lengine?

Mtu anaweza kupewa jina na wazazi wake na akalitumia jina hilo lakini majirani wanaweza kumpa jina ndugu huyo jina jipya kutokana na matendo yake. Ndugu huyo huwa na jina la nyumbani na jina la sasa la majirani. Jina linaloweza kuvuma zaidi ndiyo linaloweza kujulikana kwa wengi.

Je jina halisi la Wapare ni lipi?

Inadaiwa kuwa WAPARE jina lao halisi ni WAASU.

Mara baada ya vita hivyo waliketi pamoja na kusuluhisha mgogoro huo na ndipo huo utani ukaibuka. Katika utani huo kumekuwa na dhana kwa wachaga wakijiona wao ni wajanja mno.Wapare na wenyewe wakiijiona wajanja zaidi.

Hata wanapokutana makabila haya kabla ya kuzungumza wanaanza na neno mtani, alafu ndipo husema kilichompeleka kwa Mchaga au Mpare. Utani huo huwa unafikia hatua za matumizi ya maneno ya lugha kavu na mtani mmoja akimtukana mwingine.

Inaaminika kuwa Mchaga au Mpare muda mwingine hutaja hata maneno ya sehemu za siri za binadamu bila kutumia tafsida yoyote ile. Hata kama maneno hayo yanapotamkwa kwa kuwa mtani husema huwa hayaleti ugomvi.

Mathalani (Hashakumu si matusi) MBULA/KINU, kwa Kichaga hiyo ni sehemu ya siri ya mwanamke.

“Kishi cha meo”

Maana yake sehemu ya siri mzazi wa kike wa anayetukanwa.

Utani wa Wachaga na Wapare pia huwa katika mavazi, kwani Mchaga akimuona Mpare kavaa nguo nzuri anaweza kumpokonya na kuichukua yeye au akaichukua na kuichana chana. Wakati mwingine Mchaga / Mpare kuogopa kupokonywa nguo hizo basi huvaa nguo yake kwa kuigeuza ndani nje ili asipokonywe. Hapo uambiwa kuwa hakikisha nguo yako nzuri igeuze maana hawa watani wetu watakupokonya.

Wapare wana watani wengine ambao ni Wasambaa ambao ni jirani zao kwa muda mrefu. Inaaminika kuwa Wasambaa wakiwa katika eneo la Shambalai kuna wakati waliongozwa na Chifu Kimweri ambapo kuliwahi kutokea mgogoro baina yao, ugomvi huo ulipotatuliwa ukaongeza utani baina yao.

Wataita wanaotokea Taveta nao ni watani wa Wapare ikiaminika kuwa hata lugha zao zinafanana.

WAASU wenyewe kwa wenyewe wana utani miongoni mwa koo zao, wenyewe kwa wenyewe walipigana nia ya vita ilikuwa ni kutafuta mamlaka ya kabila hilo.Vita ilikuwa baina ya WAMBAGA na WACHONVU, WANDEME, WAMBUNGU na WAJEMA.

Ikiaminika kuwa uadui huo ulikuwa wakati wa vita tu baada ya vita kwisha tu aliyeshinda alikaa pamoja na wakawa na kiongozi mwenye nguvu sana aliyefahamika kama MFUMWA.

Inaaminika kuwa katika utani wa Wapare katika koo ambazo ni kubwa zaidi ni ule wa WAMBANGA na WACHONVU hapa ikiaminika kuwa vita vilivyopigana baina yao vilisababisha UTAWALA kuhamia kwa WAMBANGA ambao awali hawakuwa watawala.

Hapo koo zilizopambana zilifanya utani, utani ulikuwa pia kwa ndugu wa familia na hata kwa marafiki na marafiki. Mathalani utani kama ule wa kumpa mtu taarifa ya uwongo ya msiba. Kwa hiyo kama mtu asipotambua siku ya kwanza hudanganywa mara moja tu baada ya hapo atakuwa anatambua kumbe ukoo fulani ni watani wetu.

Mwanakwetu hao ndiyo ndugu zetu WAASU na utani baina yao, naomba kuweka kalamu yangu chini kwa leo. Usikose matini ijayo ambapo nitaendelea kuwatembelea WAASU.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.