Habari za Punde

Usajili wa Bodaboda waongezwa muda

 Na Kassim Abdi

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi imeamua kuongeza muda wa wiki mbili kwa usajili wa BodaBoda ili kutoa nafasi zaidi kwa wamiliki wa vyombo hivyo kukamilisha taratibu.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Rahma Kassim Ali ameeleza hayo wakati alipofanya ziara katika Afisi za Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani zilizopo Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharibi “B”.

Waziri Rahma Kassim Ali amewataka wamiliki wa Boda boda kujitokeza kwa wingi kuvisajili vyombo vyao kwa siku zilizoengezwa kwani Wizara haitatoa muda mwengine wa nyongeza baada ya wiki mbili kukamilika.

Aidha, amewataka madereva wanaoendesha bodaboda kufuata taratibu za kufanya usajili ikiwemo kuhudhuria mafunzo maalum yanayotolewa na mamlaka ya usafiri na usalama barabarani ili kufahamu vyema taratibu na sheria wakati wakiwa katika mazingira yao ya kazi.

“Niseme tu mafunzo haya yamekuwa yakisaidia sana kupunguza ajali za kila siku zinazosababisha vifo na kuleta athari kwa jamii” Alisema Waziri Rahma

Pamoja na Mambo mengine, Mhe. Rahma amewataka madereva wote wanaofika kusajili vyombo vyao kujiepusha kufanya udanganyifu wa nyaraka kwani kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria.

Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Ndugu Amour Hamili Bakari amemtaka Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama barabarani kuwasimamia watendaji wake kuongeza muda wa kuwepo kazini ili zoezi la usajali likamilike kwa haraka.

Kwa upande wao madereva wa Bodaboda wamepongeza hatua iyo ya Mhe. Waziri  kwa kuongeza muda baada ya kipindi cha Mwezi mmoja uliotolewa kumalizika.
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.