Habari za Punde

Mchezo wa Kuogolea ni Maarufu Duniani Ujio wa Kiongozi mchezo huo Utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na Shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (FINA).

 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa ujio wa Rais wa Shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (FINA) hapa Zanzibar utasaidia kwa kiasi kikubwa kuitangaza Zanzibar kiutalii hasa katika utalii wa michezo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo alipokutana na Rais wa Shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (FINA), Hussain Al Musallam akiwa na ujumbe wake wa viongozi mbali mbali wa Shirikisho hilo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwemo waliotoka Makamo makuu ya (FINA) nchini Switzerland.

Katika mazungumzo hayo Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mchezo huo ni maarufu duniani na ujio wa kiongozi huyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na Shirikisho hilo la mchezo wa kuogelea duniani (FINA).

Aliongeza kuwa hatua hiyo itaisaidia sana Zanzibar ambayo imezungukwa na bahari, na kwa vile imo katika mikakati ya kuimarisha Sera ya uchumi wa Buluu ambapo miongoni mwa malengo iliyojiwekea ni kuimarisha sekta ya utalii kwa  kupitia utalii wa michezo.

“Tumefurahishwa kwa kiasi kikubwa na ujio wa Rais wa Shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (FINA) Hussain Al Musallam ambapo kuja kwake hapa Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ushirikiano katika sekta ya michezo nchini”, alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa ujio wa kiongozi huyo ni mwanzo mzuri wa mashirikiano katika kukuza sekta ya michezo ikiwemo utalii wa michezo ambao kutokana na mazingira ya Zanzibar mafanikio makubwa yanaweza kupatikana.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ziara ya kiongozi huyo ni nafasi nzuri kwa Zanzibar kwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya michezo ambayo hivi sasa imewekewa mikakati maalum.

Alieleza haja kwa Zanzibar kuwa mwanachama wa Shirikisho hilo la Mchezo wa kuogelea duniani (FINA) hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujifunza mambo kadhaa kutoka Shirikisho hilo ambalo limepata mafanikio makubwa.

Sambama na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumkaribisha Zanzibar Rais wa Shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (FINA) Hussain Al Musallam na kumueleza mikakati na malengo yaliyowekwa na Serikali anayiongoza katika kuimarisha sekta ya michezo hapa nchini ukiwemo utalii wa michezo.

Nae Rais wa Shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (FINA), Hussain Al Musallam alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba kuogelea si mchezo tu bali ni sehemu ya maisha ambapo vijana walio wengi wamekuwa wakiufuatilia.

Alisema kuwa miongoni mwa sababu kubwa ya ziara yake ya kuja Zanzibar ni pamoja na kuja kumuunga mkono Rais Dk. Mwinyi katika mikakati yake ya kuimarisha uchumi kupitia Sera ya uchumi wa buluu ambao sekta ya utalii wa michezo imejikita ndani yake.

Kiongozi huyo wa Shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (FINA), alimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua mbali mbali zilizowekwa na Shirikisho hilo katika kuhakikisha inaweka program mbali mbali za mafunzo ya kuogelea kwa ajili ya vijana ambapo na vijana wa Zanzibar nao watafaidika.

Pamoja na hayo, Rais wa Shirikisho la mchezo wa kuogelea duniani (FINA), Hussain Al Musallam alieleza azma ya Shirikisho hilo ya kusaidia kuimarisha sekta ya utalii hapa Zanzibar hatua ambayo itaweza kuitangaza Zanzibar kimichezo Kimataifa.

Nao viongozi katika ujumbe huo walieleza kuvutiwa na mazingira ya Zanzibar ambayo yanauwezo wa kutoa vipaji kadhaa vya mchezo wa kuogelea sanjari na kuitangaza Zanzibar kiutalii kwani mchezo huo ni maarufu duniani na hapa Zanzibar umekuwa ukipendwa na vijana.

Imetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.