Habari za Punde

Utayari wa Uholanzi Kuunga Mkono Mikakati ya Pamoja na Sera ya Uchumi wa Buluu.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Balozi wa Uholanzi Nchini Tanzania Mhe. Wiebe de Boer, (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha, mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 10-3-2022.(Picha na Ikulu) 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba utayari wa Uholanzi kuunga mkono mikakati pamoja na Sera ya uchumi wa Buluu kutasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia malengo yaliyowekwa.

Rais Dk. Mwinyi amesema hayo leo Ikulu Zanzibar katika mazunguzo kati yake na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Wiebe de Boer.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza azma ya Serikali ya Uholanzi kushirikiana na Zanzibar katika kuhakikisha inaimarisha sekta zake za maendeleo ukiwemo uchumi wa ambapo nchi hiyo tayari imepiga hatua katika miongoni mwa sekta hizo.

Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Wiebe de Boer namna Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilivyoweka mikakati yake katika kuimarisha na kuuendeleza uchumi wa Buluu huku akitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Uholanzi kuja kuekeza Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimuahidi Balozi Wiebe de Boer kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji watakaoamua kuja kuekeza Zanzibar.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alipongeza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Uholanzi na kusisitiza haja ya kuongeza ushirikiano huo hasa katika sekta mbali mbali za maendeleo ukiwemo Uchumi wa Buluu.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo namna mikakati ilivyowekwa katika kuimarisha sekta nyengine za uchumi ikiwemo kilimo cha  mwani na juhudi zinazochukuliwa katika kukiimarisha pamoja na sekta ya uvuvi ambapo Zanzibar inataka iondokane na uvuvi unaofanyika hivi sasa kutokana na kutokuwa na tija wala kipato kwa wavuvi pamoja na Taifa kwa ujumla.

Nae Balozi wa Uholazi nchini Tanzania Wiebe de Boer alimueleza Rais Dk. Mwinyi  kwamba Uholanzi imekuwa na uhusiano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar tokea miaka ya sitini na kusisitiza haja ya kuimarishwa.

Balozi Wiebe de Boer alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba Uholanzi iko tayari kuiunga mkono Zanzibar katika kutimiza kiu yake ya kuimarisha uchumi kupitia uchumi wa Buluu.

Alieleza kwamba kwa vile nchi hiyo tayari imepiga hatua kubwa katika sekta za uchumi wa Buluu hivyo itahakiksiha inaiunga mkono Zanzibar ili nayo ifike pale ilipokusudia ikiwa ni pamoja na kuzishawishi Kampuni kadhaa za nchi hiyo pamoja na wawekezaji kuja kuangalia mazingira ya uwekezaji ya Zanzibar.

Balozi huyo pia, alimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua atakazozichukua katika kuhakikisha anaitangaza vyema Zanzibar kiutalii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunaandaliwa mazingira mazuri ya usafiri wa watalii kutoka nchi hiyo moja kwa moja hadi Zanzibar kupitia mashirika makubwa ya ndege ya nchi hiyo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.