Habari za Punde

Semina kuhusu usimamizi na Udhibiti wa Fedha za Umma

Mhasibu Mkuu wa Serikali Dkt. Said Seif  Mzee, akitoa nasaha na maagizo ya Usimamizi na udhibiti wa Fedha za Umma, katika Semina iliyofanyika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Baadhi ya wahasibu waliyohudhuria Semina inayohusu usimamizi na Udhibiti wa Fedha za Umma, huko Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-wakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
(PICHA NA MARYAM KIDIKO / MAELEZO)

Na Kijakazi Abdalla                    Maelezo    12/03/2022

WAHASIBU wa serikali wametakiwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kuondoa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo yao ya kazi.

Hayo yamesemwa na Mhasibu Mkuu wa serikali Dk Said Seif wakati  akifungua semina ya usimamizi na udhibiti wa fedha za umma hafla ambayo ilifanyika katika ukumbi wa sheikh Idriss  Abdul Kikwajuni .

Alisema kumekuwa na malalamiko mbalimbali yanayojitokeza katika taasisi zao jambo ambalo kwa namna moja au nyengine linasababisha kuvuruga mfumo mzima wa utekelezaji wa majukumu yao na kuishushia hadhi tasnia hiyo. 

Mhasibu huyo alisema fani ya uhasibu hivi sasa imekuwa na changamoto kubwa ikiwemo kutoaminiwa na badala yake kuonekana watu ambao wanaojali maslahi yao kwanza. 

Hata hivyo alisema kutokana na hali hiyo ipo haja hivi sasa kuwapima watendaji hao kulingana na ripoti ya mkaguzi wa ndani wa hesabu na endapo wakibaini kuna mapungufu ni vyema kujiandaa kuondoka. 

"Nimekua nikipokea malalamiko mengine kutoka kwa taasisi na idara tofauti kunitaka kuwaondosha wahasibu katika taasisi zao, hivyo imefika wakati sasa kwa wahasibu kujitambua na kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kujiepusha na hoja zilizokua hazina msingi, "alisema.

Akizungumzia umuhimu wa kutunza siri za ofisi alisema wapo baadhi ya wahasibu wamekuwa wakivujisha siri za taasisi zao jambo ambalo limekuwa likisababisha kukosekana unadhifu na uadilifu. 

Mbali na hayo aliwasisitiza watumishi hao kujiongeza kielimu ili kwenda sambamba na wakati uliyopo. 

Nae  Naibu Mhasibu mkuu wa serikali Ame Burhan aliwatka wahasibu hao kufuata miongozo ya sheria, Kanuni na taratibu za kazi zao ili kuondosha changamoto katika utekelezaji wa majukumu yao. 

Alisema zipo sheria na Kanuni tayari zimeshapitishwa katika Baraza la wawakilishi lakini wapo baadhi ya wahasibu hawazijui hivyo ni vyema kuzifatilia ili ziwasaidie katika utekelezaji wa majukumu yao.

Nao washiriki wa mafunzo hayo  wameishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapatia taalum hiyo kwani itawasaidia katika kutekeleza majukumu yao. 

Semina hiyo ya siku moja iliyowashirikisha wahasibu wa serikali jumla ya mada nne zimewasilishwa ikiwemo udhibiti wa rushwa katika usimamizi wa fedha za umma, maadili na msingi mkuu wa usimamizi wa fedha za umma, majukumu ya kusimamia fedha za umma naudhaifu wa usimamizi fedha katika taasisi za serikali. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.