Habari za Punde

Dk.Hussein Mwinyi Amewata Wadau wa Asasi za Kiraia (NGO's) KuhakikishaKila Taasisi Inatekeleza Wajibu Wake.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kufungua mkutano wa kwanza wa mwaka wa Asasi za Kiraia Zanzibar, uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Kiembesamaki Unguja nje kidogo ya Jiji la Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wadau wa Asasi za Kiraia (NGOs), kuhakikisha kila taasisi inayoanzishwa inatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia malengo yaliyobainishwa wakati wa usajili na kwa kuzingatia sheria za nchi.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo  wakati akifungua mkutano wa  Kwanza wa mwaka wa Asasi za Kiraia Zanzibar, huko katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi aliwataka wasikubali kuona kwamba sifa na malengo mema yaliyopo ya kuanzisha taasisi za kiraia yanatiwa dosari na makundi ya watu wanaojaribu kuanzisha asasi hizo wakiwa na malengo na ajenda za siri au binafsi.

Vilevile, alieleza kwamba wadau hao wanawajibu wa kuhakikisha kwamba mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma waliyoyaanzisha yanazijumuisha asasi za kiraia.

Aliwataka viongozi wa Asasi za Kiraia kuwa wabunifu katika kuendesha asasi hizo wakitambua kwamba kuna changamoto nyingi katika upatikanaji wa nyenzo na rasilimali fedha.

Aidha, aliwataka wawe wepesi wa kuandika maandiko ya miradi katika maeneo muhimu ya maendeleo ambayo wahisani katika nchi mbali mbali wako tayari kuchangia.

Pia, aliwahimiza wahisani wa ndani na nje kuendelea kushirikiana na kufanyakazi kwa karibu na asasi zilizopo hapa nchini ili ziendelee kutoa huduma kwa wananchi na kuchangia katika maendeleo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba pamoja na kutekeleza kazi zao Asasi hizo pia, zina wajibu mkubwa wa kuhakikisha amani na utulivu unaendelea kuwepo.

Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wote itakuwa pamoja na Asasi hizo za Kiraia katika kuhakikisha zinafikia malengo yaliyowekwa huku akizipongeza kwa kazi kubwa zinazofanywa na Asasi hizo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kufikiria namna ya kuanzisha Asasi zenye lengo la kuimarisha na kushirikiana na Serikali katika kuendeleza ajenda ya Serikali ya Awamu ya Nane ya Uchumi wa Buluu. “Tutahakikisha kwamba Asasi zilizoanzishwa zinatimiza malengo na matarajio ya kuanzishwa kwake”,alisema Dk. Mwinyi.

Pia, alileza kuvutiwa na kauli mbiu ya mkutano huo isemayo “Kuimarisha mashirikiano baina ya Asasi za Kiraia na Serikali kwa maendeleo ya Zanzibar”

Pamoja na hayo, aliwataka wadau wa Asasi za Kiraia kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha utoaji wa huduma za elimu, afya na maji safi na salama pamoja na kushirikiana katika kupinga vitendo vya ufisadi, rushwa na ubadhirifu wa mali za umma pamoja na udhalilishaji wanawake na watoto.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Masoud Ali Mohammed alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeziwekea mazingira mazuri Asasi za Kiraia na kuahidi kwamba Wizara anayoiongoza itaendelea kutoa msaada wake ili ile dhamira iliyowekwa na Asasi hizo iweze kufikiwa.

Nao Mabalozi kutoa Marekani Donald Wright na Balozi Didie Chassot wa Switzerland wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania kwa nyakati tofauti walieleza kwamba Serikali zao zitaendelea kuiunga mkono Zanzibar pamoja na kuziunga mkono Asasi za Kiraia zilizopo nchini.

Walieleza jinsi nchi zao zinavyosaidia katika kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo afya, elimu, demokrasia na utawala bora na nyenginezo  huku wakiipongeza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inayoendelea na malengo yake ya umoja, mshikamano na maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.

Nae Mwenyekiti wa Asasi za Kiraia Zanzibar Hassan Juma alieleza kwamba Asasi za Kiraia zitaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi kwani tayari zimeshashiriki katika masuala mbali mbali yakiwemo kuunda sera na sheria kadhaa.

Mapema Rais Dk. Mwinyi akiwa amefuatana na Mama Mariam Mwinyi alitembelea mabanda ya wadau wa Asasi za Kiraia nje ya ukumbi wa hoteli hiyo ambapo wadau hao nao walipata fursa ya kueleza shughuli wanazozifanya.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.