Habari za Punde

Waziri Mhe.Ndumbaro Ateta na Timu za Atletico Madrid, Getafe na Real Valladolid Kutangaza Utalii wa Tanzania.

 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Damas Ndumbaro ( wa pili kulia) akizungumza na Mkurugenzi wa Kilabu hiyo Antonio Sanches ( wa kwanza kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Masoko, Alberto  Heras ( wa pili kushoto)  ambao ni Viongozi  timu ya Getafe inayoshiriki daraja la kwanza (Laliga) ya Hispania. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Uhispania mwenye makazi yake mjini Paris, Ufaransa, Mhe. Samuel Shelukindo ( wa kwanza kulia)

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Damas Ndumbaro (wa kwanza kulia ) akiwa na uongozi wa timu ya Atletico inayoshiriki daraja la kwanza ( Laliga) ya Hispania wakiwa ndani ya  uwanja wa timu hiyo, Wa pili kushoto ni  Balozi wa Tanzania nchini Uhispania mwenye makazi yake mjini Paris, Ufaransa,  Mhe. Samuel Shelukindo 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Damas Ndumbaro (katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa ya Kilabu ya Atletico,Danilo Scio  mara baada ya mkutano na uongozi wa timu ya Atletico inayoshiriki daraja la kwanza ( Laliga) ya Hispania, Balozi wa Tanzania nchini Uhispania mwenye makazi yake mjini Paris, Ufaransa,  Wa pili kushoto ni Mhe. Samuel Shelukindo ( wa kwanza kulia) akiwa na  watumishi wa Ubalozi huo

Na Mwandishi Wetu, Hispania.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amefanya mazungumzo na Uongozi wa vilabu vya Atletico Madrid na  Getafe vinavyoshiriki ligi kuu nchini Hispania (Laliga) kwa lengo la kuitangaza Tanzania hususani sekta ya utalii.

Aidha, Dkt.Ndumbaro amefanya mazungumzo na Kilabu ya Real Valladolid inayomilikiwa na mchezaji wa zamani wa Kimataifa wa Brazil, Ronaldo De Lima ambapo Klabu hiyo inatarajia kupanda daraja ili kushiriki Laliga

Dkt. Ndumbaro amebainisha hayo leo Jijini Madrid alipokutana kwa nyakati tofauti na viongozi wa Vilabu hivyo vya mpira vinavyoangaliwa na mamilioni ya  watazamaji duniani.

Katika  mazungumzo hayo amesema kuwa  Viongozi wote wa Vilabu wameonesha utayari wa kushirikiana katika kuitangaza Tanzania kiutalii.

Akifafanua mazungumzo hayo Dkt.Ndumbaro amesema hiyo ni moja ya jitihada za kuhakikisha  vivutio vya Utalii vya Tanzania  vinajulikana duniani kupitia michezo kwa kutangazwa   kupitia matangazo ya  jezi ya Vilabu hivyo pamoja  na mbao za matangazo (billboards) zilizopo uwanjani

" Shabaha yetu kubwa kama nchi ni kuhakikisha tunafungamanisha utalii na michezo kwa kutumia timu kubwa za mpira  kwa lengo la kuwavutia watalii wengi zaidi kuja nchini Tanzania" amesisitiza Dkt.Ndumbaro

Ameongeza kuwa Tanzania inategemea utalii wake wa Wanyamapori  kwa asilimia 100 hivyo kupitia mkakati wa kutumia michezo vivutio vingine vya utalii kama vile utalii wa fukwe, utalii wa utamaduni pamoja na utalii wa ikolojia utaweza kujulikana dunia kote na kuwa chachu ya watalii wengi kuanza  kumiminika nchini Tanzania.

Katika mazungumzo hayo Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Uhispania mwenye makazi yake mjini Paris, Ufaransa, Samwel Shelukindo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.