Habari za Punde

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Mhe.Dk.Hussein Mwinyi Amewataka WanaCCM Kuhakikisha Wanachagua Viongozi Makini wa Mashina.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akipiga kura yake katika Shina namba moja Tawi Chama Cha Mapinduzi Kilimani Shehia ya Kilimani Unguja kumchagua Mwenyekiti wa Shina na Wajumbe, uchaguzi huo uliofanyika katika Tawi hilo Migombani leo 22-4-2022.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wananchama wa Shina namba moja Tawi la CCM Kilimani Unguja, baada ya kumaliza kupiga kura yake kumchangua Mwenyekiti na Wajumbe wa Shina namba moja Tawi la CCM Kilimani Unguja uliofanyika leo 22-4-2022.na (kulia kwa Rais) Mbunge wa Jimbo la Mpendae Zanzibar Mhe Toffiq Salim Turky

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka  wanaCCM kuhakikisha wanawachagua viongozi makini katika chaguzi za Mashina zilizoanza rasmin kwani hao ndio viongozi wapambanaji katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Rais Dk. Mwinyi ambaye pia ni a Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa  aliyasema hayo leo mara baada ya kushiriki kikamilifu katika upigaji wa Kura za Mabalozi na Wajumbe katika Shina namba Moja la Migombani Mjini Unguja, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Rais Dk. Mwinyi, alieleza kwamba ni vyema wakachaguliwa watu makini ambao wanaweza kusaidia  kufanya kazi ndani ya chama hicho na wasidharau chaguzi hizo kwani katika hatua hiyo viongozi wa Shina ndio wapambanaji na ndio wenye watu.

Alisema kuwa uchaguzi rasmi umeanza katika chama hicho cha CCM ambayo ni hatua awali katika ngazi za Mashina zoezi ambalo litaendelea katika ngazi zote kuanzia Shina, Wadi, Wilaya, Mkoa  hadi Taifa.

Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa kupewa fursa hiyo ya kushiriki kikamilifu katika kumchagua Balozi wa Shina hilo namba moja la Migombani ambapo alitumia nafasi hiyo kukiombea Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kiweze kufanikiwa katika chaguzi zake zote zinazoendelea.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi  aliwashukuru wanaCCM wa Shina hilo namba moja la Migombani kwa kumpokea vizuri akiwa mwanachama mpya wa Shina hilo kwani tokea baada ya uchaguzi wa Dola uliopita amekuwa mkaazi rasmi wa Shehia ya Migombani.

“Hili ndio Shina langu na leo nimefurahi kushiriki uchaguzi katika Shina hili....tutambue kwamba tunaowachagua mwaka huu ndio watakaokuwa wapambanaji wetu katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025 ”,alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Nao wanachama wa CCM wa Shina hilo walitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kushiriki katika uchaguzi huo ambapo waliahidi kufanya uchaguzi wa haki na wenye amani na usalama kwa azma ya kukiendeleza na kukiimarisha chama chao ili kiendelee kushika Dola.

Katika uchaguzi huo wanowania nafasi za Mwenyekiti wa Shina ni  Tatu Simai Faki na Canada Moris Marekani pamoja na Wajumbe watano kwa nafasi nne za Ujumbe wa Shina hilo zilizopo.

Uchaguzi wa Mashina ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeanza rasmi kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho na baada ya kumaliza chaguzi hizo uchaguzi unaofuata ni wa Matawi na hatimae kuendelea katika ngazi nyengine hadi ngazi ya Taifa.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.