Na.Abdulrahim Khamis.OMPR. 18/04/2022
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito huo akifungua Tamasha la Ramadhani lililotayarishwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja lililofanyika katika kiwanja cha Misuka Mahonda.
Amesema Zanzibar inasifika kwa maadili mema kihistoria yaliyotokana na Dini ya Kiislamu maadili ambayo kwa sasa yamepotea hatua inayopelekea kukosa viongozi bora wenye hapo baadae.
Amesema umefika wakati wazazi na walezi kurudi katika malezi ya Asili ambayo yataweza kuisaidia Serikali katika kuondosha matendo maovu.
Amesema malezi mema kwa watoto yatasaidia kupata Wanazuoni na Maimamu wa baadae ambao watakuja kuisimamia Dini ya Allah (S.W) ambao pia watasaidia kupata Zanzibar yenye viongozi bora wenye maadili mema.
Aidha Alhajj Hemed amesema kuwa ana Imani Kongamano hilo litakuwa na mnasaba wa Maendeleo ya Zanzibar yenye maadili mema kupitia mada mbali mbali na ujumbe utakaotolewa kwa wawasilishaji mbali mbali.
Sambamba na hayo Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuwataka waumini wa Dini ya Kiislamu kuendeleza Ibada mbali mbali na kujifunza mengi mazuri yanayopatikana katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Muhamed Mahmoud ameeleza kuwa lengo la kuandaa Tamasha hilo ni kubadiki fikra za wananchi wa Mkoa wa Kaskazini na Zanzibar Unguja kwa ujumla ili Zanzibar irudi katika maadili iliyokuwa ikisifika.
Amesema Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja imeanzisha Programu mbali mbali kila mwezi ambazo lengo ni kuwaelimisha wananchi wa Mkoa huo kufahamu mengi mazuri ya kuwa nayo ambayo yatapelekea kuwa na Zanzibar yenye Maendeleo na kuisaidia Serikali katika kufikia malengo yake iliyojiwekea.
Nae Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi amesema ili kurudi katika malezi bora ni wajibu kufuata maelezo yaliyomo katika Qur-an Tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W) na kushauri kuundwa kwa Kamati za Maadili katika Shehia.
Tamasha la Ramadhani lililoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja litajumuisha matukio mbali mbali ikiwemo Kongamano, Mashindano ya Kuhifadhi Qur-an, Ugawaji wa Sadaka kwa kaya Maskini pamoja na Iftaari kwa makundi mbali mbali.
No comments:
Post a Comment