Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Said Suleiman akimsikiza kwa makini Meneja msimamizi mafunzo wa Kituo cha Tiba na Marekebisho ya tabia kilichopo Kidimni ndugu Simai M. Amour alipokuwa akimuelezea ratiba ya mzunguko wa maisha ya wanafunzi waliopo kituoni hapo.
Kituo
cha Tiba na Marekebisho ya tabia kilichopo Kidimni kinatarajiwa kuwa ni kitovu
cha malezi ya vijana walioathirika na matumizi ya Dawa za Kulevya sehemu ambayo
watapatiwa tiba sahihi na stadi za maisha, kujifunza masuala mbali bali yenye
manufaa ili waendane na harakati za maendeleo kama mipango ya Serikali
ilivyobainisha
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Said Suleiman ameyasema
hayo wakati alipotembelea kituo hicho akiwa ameongozana na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar Kanali Burhani Z. Nasoro pamoja na
viongozi wengine wa mamlaka hio
Mhe Harusi amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatekeleza mradi huu
ikiwa imetumia busara kubwa na kufikiria wananchi wake hasa vijana ambao ndio wajenzi
na rasilimali muhimu katika kuendeleza uchumi wa nchi na taifa kwa ujumla
Amesema dawa za
kulevya ni adui wa maadili, ndio chanzo cha maasi na huharibu mfumo wa uchumi,
hivyo ameiomba jamii kuunganisha nguvu za pamoja kuchukia matumizi ya dawa za
kulevya kwa kuwafichuwa waingizaji, wasambazaji na wauzaji
“Wajibu wetu wananchi kila mmoja wetu kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuwafichua wafanyabiashara na wasambazaji wa dawa za kulevya”alisisitiza Bi Harusi
Mhe Harusi akiwa kituoni hapo amekagua na kutembelea mradi wa banda la malisho ya ngombe, mabanda ya kuku, sehemu inayotegemewa kujengwa karakana ya kutengeneza magari, sehemu inayolimwa bustani za mbogamboga, vyumba vya kulala na ofisi
Nae na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar Kanali Burhani Z. Nasoro
amemuhakikishia Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Said Suleiman kuendelea
kuweko kwa ulinzi na usimamizi
madhubuti katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ndani na nje ya
kituo hicho
Aidha Kanali Burhani amewasisitiza wazazi na wanafamilia kupeleka vijana wao katika Kituo cha Tiba na Marekebisho ya tabia kilichopo Kidimni kwani kuna fursa muhimu za kijana kuweza kujitegemea mara tu atakapotoka hapo na kuwa raia wema wa baadae.
No comments:
Post a Comment