Habari za Punde

Vyombo vya Ulinzi na Usalama Kushirikiana na Waandishi wa Habari.- DC. Kunambi.

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi "A" Mha Suzan Peter Kunambi akifungua mdahalo kati ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama na Waandishi wa Habar, kuhusu majadiliano ya usalama wa waandishi wa habari huko katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC).

Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja  na Waandishi wa Habari,wakijadili  usalama wa waandishi wa habari huko katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC)

Picha na  Khadija Khamis -Maelezo Zanzibar,

Na Khadija Khamis Maelezo Zanzibar ,01/05/2022.

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mhe,Suzan Peter Kunambi  amewataka watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana na waandishi wa habari katika utekelezaji wa kazi zao ili kupatikana taarifa zenye uweledi na usahihi.

 

Hayo ameyasema huko katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) Kijangwani wakati akifungua mdahalo wa kujadili usalama wa waandishi wa habari na mahusiano na vyombo vya ulinzi na Usalama kwa Jeshi la PolisI, Vikosi vya SMZ pamoja na Waandishi wa habari .

 

Amesema mdahalo huo utajenga mahusiano mazuri kati ya vyombo vya habari na jeshi la polisi ambao utasaidia   utoaji wa taarifa sahihi na zenye vyanzo vinavyoeleweka  ikizingatia kwamba utekelezaji wa kazi zao unategemeana .

 

Akitoa nasaha kwa waandishi wa habari kutumia maadili ya uandishi katika kazi zao na kuhakikisha taarifa wanazozitoa wamezipata katika vyanzo sahihi na kuzifanyia uchunguzi ili kuepusha mgongano ambao uko kinyume na sheria .

 

Akitoa wito kwa Jeshi la Polisi  kwamba kuwa na utayari wa kutoa taarifa katika wakati  sahihi  jambo ambalo litaepusha kutoka taarifa kinyume na uhalisia katika mitandao ya kijamii .

 

Nae Mratibu  Msaidizi wa Polisi, Said Mohd Said  akitoa maelezo katika Mdahalo huo kwa Niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, amesema mahusiano kati ya Jeshi la Polisi pamoja na waandishi wa habari ni suala ambalo haliepukiki kwani hushirikiana katika kuitumikia jamii hivyo ni vyema kudumisha mahusiano hayo.

 

Akiwasilisha mada kuhusu uhusiano kati ya Polisi na Waandsishi wa habari, ASP. Ramadhan Himid  kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar amasema ni vyema kufanyakazi kwa kuaminiana baina ya vyombo hivi sambamba na kufuata sheria .

 

Alifahamisha  kuwa na mashirikiano ya pamoja kati ya Waandishi wa Habari na Jeshi la Polisi kutasaidia utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi .

 

 Nae Mwaandishi Muandamizi Dk Saleh Mnemo amesema iwapo kila mmoja ataheshimu wajibu wa mwenzake  pamoja na kuulinda uhuru wa vyombo vya habari kutasaidia usalama kwa Waandishi wa habari.

 

Mdahalo huo wa siku moja ni sehemu ya  utekelezaji wa mradi wa Usalama wa waandishi wa habari unaotekelezwa kwa pamoja na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)  na Shirika la International Media Support (IMS) ambao umewashirikisha Maofisa wa Jeshi la Polisi, Maofisa wa Vikosi vya Idara Maalum SMZ pamoja na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.