RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein
Ali Mwinyi amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance
Salvatory Mabeyo kwa kutekeleza vyema majukumu yake katika kipindi chake chote
cha utumishi ndani ya Jeshi hilo.
Rais Dk.
Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya
Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo ambaye amefika Ikulu
Zanzibar kwa ajili ya kumuaga Rais kufuatia kumaliza muda wa utumishi wake
ndani ya Jeshi hilo mwishoni mwa mwezi huu.
Katika maelezo
yake Rais Dk. Mwinyi alimuelezea Jenerali Mabeyo kwamba ni kiongozi ambaye
alifanya kazi zake vyema katika Jeshi hilo na alimpa ushirikiano mkubwa yeye na
viongozi wenzake wakati akiwa Waziri wa Ulinzi hatua ambayo ilimuwezesha kutekeleza
mambo mengi ndani ya Jeshi hilo.
Alieleza kwamba
ushirikiano alioupata kutoka kwa Jenerali Mabeyo wakati akiwa Waziri wa Ulinzi
na hata akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anauthamini
na ataendelea kuukumbuka.
Hivyo, Rais
Dk. Mwinyi alimtakia kila la kheri Jenerali Mabeyo katika maisha yake ya
kustaafu hasa ikikumbukwa kwamba amelitumikia kwa muda mrefu Jeshi hilo na
kufanya mambo mengi yatakayoacha alama.
Sambamba na
hayo, Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Jenerali Mabeyo kwa mashirikiano yake
aliyoyatoa katika kuhakikisha changamoto mbali mbali zinapatiwa ufumbuzi wakati
wa uongozi wake ndani ya Jeshi hilo.
Pamoja na
hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zote
mbili kwa mashirikiano ya Jeshi la Ulinzi Tanzania katika kutafuta ufumbuzi wa
kudumu wa changamoto za ardhi katika maeneo ya Jeshi.
Alitoa
shukurani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga Bajeti
maalum kwa ajili ya fidia hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana
kwa ufumbuzi wa kudumu katika changamoto hiyo.
Mapema Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo alitoa pongezi na
shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kutekeleza vyema uongozi wake uliotukuka
tokea akiwa Waziri wa Ulinzi hadi hivi sasa akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi.
Jenerali
Mabeyo alitumia fursa hiyo kwa kumuaga rasmi Rais Dk. Mwinyi kufuatia kumaliza
muda wake wa utumishi ndani ya Jeshi hilo utakaokamilika mwishoni mwa mwezi
huu.
Katika maelezo
yake Mkuu huyo wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania alieleza haja ya kuja kumuaga
pamoja na kutoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi na kueleza kuwa ni kiongozi
ambaye amefanya kazi nae kwa muda mrefu na kumsaidia katika kutekeleza vyema
majukumu yake ndani ya Jeshi hilo.
“Nakutakia
afya njema na maisha marefu Mheshimiwa Rais pamoja na familia yako….nathamini
sana ushirikiano ulionipa katika kipindi chako cha uongozi tokea ukiwa Waziri
wa Ulinzi hadi leo hii, ahsate sana”, alisema Jenerali Mabeyo.
Mkuu huyo wa
Majeshi ya Ulinzi Tanzania alisema kuwa Jeshi la Ulinzi Tanzania litaendelea
kumkumbuka Rais Dk. Mwinyi kwa busara na hekima zake katika kuzishughulikia
changamoto mbali mbali ndani ya Jeshi hilo ambalo hatimae limepata mafanikio
makubwa.
Alieleza
kwamba katika uongozi wake Rais Dk. Mwinyi akiwa Waziri wa Ulinzi aliweza
kutatua changamoto kadhaa sambamba na kulifanyia mambo mengi Jeshi hilo hatua
ambayo imepelekea viongozi wa Jeshi hilo waendelee kufuata nyayo zake.
Alipongeza
hatua zinazoendelea kuchukuliwa katika kutatua changamoto za ardhi na kueleza matarajio
yake ya mafanikio yatakayopatikana katika kupata ufumbuzi wa kudumu wa
changamoto hiyo.
Sambamba na
hayo, alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa busara na hekima kubwa anayoendelea
kutumia katika kuitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto hiyo ya ardhi hasa kwa
kutambua kwamba Jeshi ni sehemu ya wananchi.
Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,
Ikulu Zanzibar. RESPONSIBILITY
No comments:
Post a Comment