Habari za Punde

Waziri Mhe.Mchengerwa Ataja Makubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Katika Michezo Wakati wa Wazinduzi wa Mbio za CRDB Marathon Ajisajili.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania Mhe, Mohamed Mchengerwa akikabidhiwa namba yake ya usajili wa Mbio za Kimataifa ya CRDB Marathon na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB.Bi.Tully Esther Mwambapa.wakati wa halfa ya uzinduzi wa Msimu wa Tatu Mbio za Kimataifa za CRDB uliofanyika katika viwanja vya Nyerere Jijini Dodoma.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania Mhe, Mohamed Mchengerwa akizindua Mbio za Kimataifa za CRDB Msimu wa Tatu katika viwanja vya Nyerere Jijini Dodoma.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania Mhe, Mohamed Mchengerwa akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mbio za CRDB wakati wa halfa ya uzinduzi wa Msimu wa Tatu Mbio za Kimataifa za CRDB uliofanyika katika viwanja vya Nyerere Jijini Dodoma.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania Mhe, Mohamed Mchengerwa akijumuika na Wafanyakazi wa Benki ya CRDB na Wanamichezo wakiwa katika mazoezi ya viungo, wakati wa halfa ya uzinduzi wa Msimu wa Tatu Mbio za Kimataifa za CRDB uliofanyika katika viwanja vya Nyerere Jijini Dodoma.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania Mhe, Mohamed Mchengerwa akizungumza wakati wa halfa ya uzinduzi wa Msimu wa Tatu Mbio za Kimataifa za CRDB uliofanyika katika viwanja vya Nyerere Jijini Dodoma.

Na John Mapepele.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekua mstari wa mbele siyo tu katika  kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika michezo  bali inashiriki moja kwa moja kuwekeza katika michezo kwa  kuwa inaamini kuwa michezo ni uchumi na biashara ambayo inatoa ajira nyingi kwa vijana.

Mhe. Mchengerwa amesema hayo leo Mei 5, 2022 kwenye uzinduzi wa msimu wa tatu wa mbio za kimataifa za CRDB kwenye viunga vya Nyerere jijini Dodoma ambapo amewataka wakuu wote wa mikoa na wilaya nchi nzima kuhamasisha michezo kwenye maeneo yao ili kusaidia wananchi kujenga afya, kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza na kuinua uchumi wao na taifa kwa ujumla. 

Aidha, amewaelekeza maafisa michezo na utamaduni katika kila mkoa na wilaya kuratibu mazoezi na mashindano ya michezo na sanaa ili kubaini na kuwatambua watanzania wenye vipaji kupitia program iliyoanzishwa na Serikali ijulikanayo kama mtaa kwa mtaa ili kuwanyanyua wafike kwenye kiwango cha kimataifa, ambapo amesema tayari Serikali  imetenga fedha  kwa ajili ya kazi hiyo. 

 “Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Mhe. Rais  Samia ameweka misingi, na mikakati iliyojikita katika masuala kadhaa ya muhimu ikiwemo nyongeza ya bajeti ya Wizara, punguzo au kuondolewa kwa kodi ya nyasi bandia ili kuimarisha viwanja vya soka pamoja na kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya michezo nchini. 

 Mfuko huo umepewa chanzo madhubuti ambacho ni fedha za asilimia tano 5% ya mapato yatokanayo na michezo ya kubashiri matokeo ya michezo (Sports Betting)” amesisitiza Mhe Mchengerwa.

Amefafanua kuwa, Mhe. Samia  ameelekeza kuwa mfuko huo ukasaidie shughuli mbalimbali za michezo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha timu za Taifa zinahudumiwa na kuratibiwa ipasavyo, miundombinu ya michezo inaboreshwa na kujengwa, wataalamu wa michezo wanapewa mafunzo yanayostahili ikiwa ni pamoja na makocha ili kuendana na hali halisi halisi Duniani. 

Kwa upande wa sekta za Utamaduni na Sanaa amefafanua kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya sanaa, mwaka huu wasanii  wameanza kunufaika kwa kupokea mirabaha kutokana na kazi zao za sanaa, ambapo amesema kumekuwa  changamoto chache ambazo zinafanyiwa kazi sambamba na kuzingatia maelekezo aliyoyatoa Mhe. Rais Mei 31 mwaka huu wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Muziki wa Hiphop la “The Dream Concent” Jijini Dar es Salaam. 

Amesisitiza kuwa tayari Serikali imeanza ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya kuja kuratibu mashindano ya kimataifa hususan mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027 ambapo amewaomba wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na CRDB kushirikiana na Serikali katika kujenga  miundombinu.

 “Kama Wizara tumejipanga kuhakikisha ndoto za Mhe. Rais Samia na watanzania kwenye michezo zinatimia kwa sisi kufanya vizuri, nimeshawambia wenzangu kuwa mimi kama Waziri mwenye dhamana sitakubali  kupokea sababu zisizo na msingi kuhusu kwa nini tunafanya vibaya kwenye michezo ”amesisitiza, Mhe. Mchengerwa. 

Pia amesema Serikali imerejesha Tuzo kubwa kabisa za Filamu pamoja na Muziki Tanzania zilizofanyika Disemba, 2021 na mwanzoni mwa mwezi Aprili 2022 ambapo amesisitiza kuwa kurejea kwa tuzo hizo kunatoa hamasa kwa wasanii kuendelea kutoa kazi zenye ubora zaidi ambazo pamoja na kuwaingizia kipato zitachangia kutangaza nchi yetu katika ngazi ya kimataifa.

Aidha amewahimiza wanamichezo na wadau wa michezo wote kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ya watu na makazi, litakalofanyika tarehe 23 Agosti, 2022.

Katika uzinduzi  huo amekuwa mtu wa kwanza kujisajili kukimbia kilomita 42.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.