Habari za Punde

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango Amekutana na Kuzungumza na Diaspora Nchini Sweden.Akiwa katika ziara Yake.

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza na  viongozi wa vyama mbalimbali vya watanzania waishio nchini Sweden wakati alipokutana  na viongozi hao mjini Stockholm nchini Sweden.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewaasa watanzania  waishio nchini Sweden pamoja na maeneo mengine duniani (Diaspora) kuwa na mshikamano pamoja na maelewano ili waweze kutatua changamoto zao zinazowakabili pamoja na kuchangia ujenzi wa taifa lao la Tanzania.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipofanya mazungumzo na viongozi na wawakilishi wa vyamba mbalimbali vya watanzania waishio nchini Sweden. Amesema serikali inathamini mchango mkubwa unaotolewa na diaspora katika kufanikisha adhma ya diplomasia ya uchumi hivyo wanapaswa kuondoa tofauti zao na kuendelea kuitangaza vema Tanzania nchini Sweden.

Pia amewataka kuheshimu katiba za vyama vyao wanavyoviongoza  nchini Sweden pamoja na kukutana na kujadili kwa uwazi kwa kuzingatia katiba waliojiwekea katika kuendesha mambo yao.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Diaspora ni sehemu muhimu ya Tanzania, kwani serikali inathamini sana utaalamu, biashara na utangamano unaoleta manufaa kwa familia zao pamoja na taifa kwa ujumla.

Aidha Makamu wa Rais amewahakikishia kuwa serikali inaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo za uwekezaji, utalii pamoja na biashara. Amesema suala la Hadhi Maalum kwa wanadiaspora, serikali ya awamu ya sita  inaendelea kulifanyia kazi kwa kuzingatia maoni yaliotolewa na kuwaahidi suala hilo kushughulikiwa kikamilifu na kwa wakati.

Makamu wa Rais ameupongeza  Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa watanzania waishio nchini Sweden na maeneo mengine ya uwakilishi.

Kwa upande wao, wawakilishi wa vyama mbalimbali vya wanadiaspora nchini Sweden, wameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuteua watumishi waadilifu na wachapa kazi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden. Aidha wameiomba serikali kushughulikia kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo mazingira bora ya kufanya biashara, changamoto katika sekta ya utalii, pamoja na changamoto za  huduma za kifedha wanazopata katika mabenki mbalimbali nchini Tanzania.

Aidha wanadiaspora hao wamemueleza Makamu wa Rais jitihada mbalimbali wanazozifanya katika kuchangia ujenzi wa taifa kama vile uwekezaji katika sekta ya ufugaji, biashara, elimu  pamoja na kilimo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akisikiliza maoni kutoka kwa viongozi wa vyama mbalimbali vya watanzania waishio nchini Sweden wakati alipofanya mazungumzo na viongozi hao mjini Stockholm nchini Sweden.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akisikiliza maoni kutoka kwa viongozi wa vyama mbalimbali vya watanzania waishio nchini Sweden wakati alipofanya mazungumzo na viongozi hao mjini Stockholm nchini Sweden.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango akiwa katika picha ya pamoja na  watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden pamoja na  viongozi wa vyama mbalimbali vya watanzania waishio nchini Sweden mara baada ya mazungumzo na viongozi hao yaliofanyika  mjini Stockholm nchini Sweden.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.