Habari za Punde

HESLB yaanza kuwadai TZS 10.6 bilioni waliokopeshwa ‘Law School’

Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo Tanzania (LST) Jaji Dkt. Benhajj Masoud na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Bardu wakiweka saini hati ya makubaliano yatakayoiwezesha HESLB kudai zaidi ya TZS 10.6 bilioni kutoka kwa wanufaika 5,065 waliokua wanafunzi wa taasisi hiyo kati yam waka 2008 na 2015. Hafla hiyo ilifanyika leo (Jumanne, Juni 21, 2022) Jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia ni Wanasheria wa Taasisi hizo, Abdallah Mtibora (kushoto) na Belinda Mollel.

1   Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru na Mkuu wa Taasisi ya Mafunzi ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) Jaji Dkt. Benhajj Masoud wakibadilishana hati ya makubaliano yatakayoiwezesha HESLB kudai zaidi ya TZS 10.6 bilioni kutoka kwa wanufaika 5,065 waliokua wanafunzi wa taasisi hiyo kati ya mwaka 2008 na 2015. Hafla hiyo ilifanyika leo (Jumanne, Juni 21, 2022) Jijini Dar es Salaam. Pembeni ni Wanasheria wa Taasisi hizo, Abdallah Mtibora (kushoto) na Belinda Mollel.

 Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa vitendo Tanzania (LST) Jaji Dkt. Benhajj Masoud (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Bardu (kushoto) wakionesha hati ya makubaliano yatakayoiwezesha HESLB kudai zaidi ya TZS 10.6 bilioni kutoka kwa wanufaika 5,065 waliokua wanafunzi wa taasisi hiyo kati ya mwaka 2008 na 2015. Hafla hiyo ilifanyika leo (Jumanne Juni 21, 2022) Jijini Dar es Salaam. 

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam                                                                                                                      

Wanasheria 5,065 waliokopeshwa zaidi ya TZS 10.6 bilioni kama mikopo wakiwa wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria Tanzania (Law School of Tanzania - LST) sasa watapaswa kurejesha mikopo hiyo kwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

 

Wanasheria hawa ni wale walionufaika na mikopo ya elimu wakiwa wanafunzi wa LST kati ya mwaka 2008 na 2015 wakisoma Stashahada ya Juu ya Uanasheria kwa Vitendo (Post Graduate Diploma in Legal Practice) wakati Sheria ya HESLB ilipokua hairuhusu wanafunzi wa LST kukopeshwa. Sheria ya HESLB ilirekebishwa mwaka 2014 na kuruhusu wanafunzi wa LST kukopeshwa na HESLB.

 

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyosainiwa jijini Dar es salaam leo (Jumanne, Juni 21, 2022) na Watendaji Wakuu wa taasisi hizo, wanasheria hao ni wale waliosoma kupitia kundi (cohort) la kwanza hadi 19 na kukopeshwa na Serikali kupitia LST.

 

“Tunashukuru kuwa mikataba waliyosaini walipokua wanafunzi-wanasheria ipo wazi kuwa LST inaweza kuipa kazi ya kukusanya madeni haya taasisi yoyote ya umma au binafsi … na hivyo baada ya mazungumzo tangu 2019, leo tumefikia hatua hii,” amesema Jaji Dkt. Benhajj Masoud, Mkuu wa LST katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema HESLB ina uzoefu na utayari wa kutekeleza jukumu hilo na kuwakumbusha wanufaika hao kujitokeza na kurejesha.

 

“Tumejipanga kuanza kuwahudumia kuanzia Julai 1, 2022 … hivyo tunatoa wito kwa wateja wetu hawa kurejesha fedha hizi pamoja na zile walizokopeshwa wakiwa wanafunzi wa shahada za kwanza ili ziwanufaishe vijana wengine wa kitanzania wanaohitaji,” amesema Badru.

 

HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu makuu mawili, kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wa elimu ya juu na pia kukusanya fedha za mikopo zilizoiva ambazo zimezotolewa na Serikali kwa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu tangu mwaka 1994/1995.

 

Mwisho.

 

Imetolewa na:

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu

DAR ES SALAAM

Juni 21, 2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.