Habari za Punde

Jumuiya ya Istiqaama Zanzibar Yapongezwa kwa Kuunga Mkono Juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Jumuiya ya Istiqaama Zanzibar, walipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha na kuelezea Kazi zinazofanywa na Jumuiya hiyo kwa Jamii, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 4-6-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Jumuiya ya Istiqama Zanzibar kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwahudumia wananchi.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na viongozi pamoja na Wanajumuiya wa Jumuiya ya Istiqama Zanzibar ikiwa ni muendelezo wake wa kukutana na Jumuiya pamoja na  Madhehebu mbali mbali ya Kidini yaliyoapo hapa Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa Jumuiya hiyo na kueleza kwamba Serikali imekuwa ikifarajika kwa taasisi za kidini na zisizo za kidini kwa kuiunga mkono katika kuwasaidia wananchi kwa kutoa huduma za jamii katika mambo mbali mbali.

Alitoa shukurani kwa Jumuiya hiyo kwa kuhubiri amani sambamba na kutoa huduma mbali mbali za kijamii zikiwemo maji, elimu, afya huku akitoa pongezi kwa kazi hiyo ya kumridhisha Mwenyezi Mungu na kuisaidia Serikali na kueleza haja ya kuikuza na kuipanua zaidi ili kuisaidia Serikali na wananchi kwa ujumla.

Rais Dk. Mwinyi alituia fursa hiyo kusisitiza amani ambayo inatokana na utulivu katika jamii na imani zao za kidini ambapo kazi ya kuielemisha jamii masuala ya kidini na umuhimu wa kuwa raia wema husaidia kuleta utulivu nchini.

Alieleza kwamba Serikali itakuwa tayari kutoa msaada wake pale utakapohitajika huku akisisitiza kwamba milango yake iko wazi wakati wote.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alipokea changamoto kadhaa za Jumuiya hiyo ikiwemo ya barabara ya kuelekea skuli ya Mahadi Istiqama Tunguu inayoanzia barabara kuu ya Tunguu na kuahidi kuzifanyia kazi na kuifungua barabara hiyo pale ujenzi wake utakapokamilika.

Pia, alitoa ufafanuzi juu ya suala zima la kodi zinazotolewa kwa biadhaa zinazoletwa na Jumuiya zikiwemo zile za msaada ama za biashara na kuahidi kuangaliwa ujumla wake kwa kukaa pamoja kati ya Jumuiya hiyo na Wizara husika ya Fedha na Mipango ili kupata ufumbuzi zaidi juu ya suala hilo.  

Akizungumzia suala zima la maadili, Rais Dk. Mwinyi alieleza juhudi zilizochukuliwa na Serikali katika kupambana na udhalilishaji ikiwemo kuweka mahakama maalum na kuondoa dhamana kwa wanaofanya makosa ya udhalilishaji huku akisisitiza kutolewa elimu zaidi kwa Jamii juu ya kadhia hiyo hasa elimu ya dini.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Istiqama Zanzibar Salum Nassor Salum alitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa niaba ya Jumuiya hiyo kwa ukaribu alionao kwa Jumuiya hiyo pamoja na kutimiza ahadi yake ya kukutana na Jumuiya na madhehebu mbali mbali ya kijamii.

Alieleza jinsi Jumuiya hiyo inavyopata mashirikiano makubwa kutoka kwa Serikali anayoiongoza Rais Dk. Mwinyi na viongozi wake wote.

Alieleza kwamba Jumuiya hiyo ni taasisi ya Kiislamu ya Kiibadhi ya kheri na kijamii na isiyo ya kisiasa wala kibiashara ambayo malengo yake makubwa ni kuhudumikia Jamii ya Wazanzibari kwa ujumla.

Aliongeza kuwa lengo jengine ni kuchangia katika kutengeneza jamii yenye kujifahamu kupitia sekta ya elimu na kuifanya Jamii kukua vizuri kimaadili na kitaaluma.

Alisema kuwa Jumuiya hiyo imekuwa na lengo la kutoa huduma bora za afya hasa kumlenga mwanamke na mtoto, kutoa huduma mbali mbali za kijamii kwa lengo la kukidhi haja za wahitaji ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wale ambao wamejaaliwa uwezo katika kutekeleza wajibu wao wa kusaidia wahitaji.

Naibu Katibu Mkuu huyo alizieleza kazi kubwa za Jumuiya ambazo zimegawika katika sekta ya elimu, afya na huduma za kijamii ambapo kwa upande wa sekta ya elimu Jumuiya hiyo ina vitengo vya Madrasa za Quran, Mahad ya sharia za dini pamoja na skuli iliyopo Tunguu yenye jumla ya wanafunzi 921 na walimu 63.

Kwa upande wa sekta ya afya alieleza kuwa Jumuiya hiyo inatoa huduma za afya kupitia hospitali yake ya Al Rahma iliyopo Kilimani ambayo imejengwa mwaka 2000 inayotoa huduma mbali mbali kikiwemo kitengo maalum cha huduma za akina mama ambao wanahudumiwa na madaktari wanawake.

Alizieleza huduma nyengine kadhaa zinazotolewa na Jumuiya hiyo ikiwemo kusafirisha mahujaji wanaokwenda kutekeleza ibada ya Hijja nchini Saud Arabia, huduma za kuchimba visima, kutoa huduma za vyakula vya futari wakati wa mwezi wa Ramadhani, ujenzi wa misikiti pamoja na usimamizi wake.

Aidha, alisema kuwa Jumuiya hiyo inatambua na kuthamini juhudi kubwa za Serikali katika kutoa fursa za ajira kwa wananchi na imekuwa chachu ya kuchagia maendeleo ya nchi kwa kuweza kutoa fursa za ajira kwa wananchi ambapo kwa sasa ina wafanyakazi 495 katika sekta zote wote wakiwa ni wazawa wanaofaidika na ajira hizo.

Alisisitiza kwamba Jumuiya hiyo ina matumaini makubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuleta maendeleo ya nchi na wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuimarisha amani, utulivu, umoja na mshikamano kwa wananchi.

Sambamba na hayo, Wanajumuiya ya Istiqama Zanzibar walitumia fursa hiyo kueleza jinsi wanavyofarajika na juhudi anazozichukua Rais Dk. Mwinyi katika kuwaongoza Wazanzibari wote na kuahidi kuendelea kumuunga mkono.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.