Habari za Punde

Mradi wa Ng’ombe wa Kisasa wa Maziwa wa Kupaisha Wafugaji Mbeya

Na Georgina Misama – MAELEZO, Mbeya.

Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kumkomboa mtanzatia kiuchumi kila mmoja kwa nafasi yake, kuanzia wafanyakazi, wafanyabiashara bila kuwaacha wakulima na wafugaji ambapo hivi karibuni kwa kushirikiana na Sekta binafsi imeanziasha mradi mkubwa wa ng’ombe wa kisasa wa maziwa Jijini Mbeya.

Mradi huo umehusisha kuwaleta ng’ombe ambao ni maalumu kwa uzalishaji wa kiwango kikubwa cha maziwa kutoka nchi ya Afrika Kusini ambapo inakadiriwa kuwa ng’ombe mmoja ana uwezo wa kutoa mpaka lita 30 za maziwa kwa siku ukilinganisha na ng’ombe wa asili ambao kiwango chao cha juu cha maziwa kwa siku ni lita 10.

Akizungumzia mradi huo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Omela amesema kwamba anaishukuru  Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwani imewatendea makuu mkoa wa Mbeya ikiwemo kushirikiana na Sekta Binafsi na kuwapelekea mradi wa ng’ombe wa kisasa wa maziwa.

“Baada ya kupokea mradi huu wa ng’ombe wa kisasa wa maziwa kutoka Afrika Kusini, utatufanya Mbeya tuwe wazalishaji wakuu wa maziwa katika nyanda za juu kusini na kaskazini, mpaka sasa tayari tuna viwanda vidogo vya kuchakata maziwa zaidi ya 19,” alisema Mhe. Omela.

Aliongeza kwamba baadhi ya wawekezaji binafsi katika sekta ya maziwa kama vile kampuni ya ASAS inapata maziwa mengi kutoka mbeya kwa ajili ya viwanda vyake vilivyopo mkoni Iringa hii ni kutokana na Mbeya kutoa kiwango kikubwa cha maziwa.

Ikumbukwe Serikali imeshirikiana na Benki ya Wakulima Tanzania (TADB) katika kuhakikisha mradi huu unawafikia wakulima na wafugaji walipo Mbeya, hususan wafugaji wa Wilaya ya Buswekelo ambao tayari walishakuwa na uzoefu katika ufugaji hasa wa ngombe wa nyama na maziwa hivyo mradi huu umewaongezea ujuzi na kuwaletea mapinduzi katika uzalishaji wa maziwa.

Meneja wa Benki ya Wakulima Tanzania (TADB) kutoka Nyanda za Juu Kusini Alphonce Mukoki alisema kwamba mpaka sasa takribani ng’ombe 84 wameshafikishwa na kukabidhiwa kwa wafugaji wa eneo la Buswekelo ambao tayari walipatiwa mafunzo ya namna ya kuwatunza ng’ombe hao na wanapokea huduma za wataalamu wa mifugo kutoka serikalini ili kuhakikisha wanafuga kibishara na si kwa mazoea kama ilivyokuwa awali.

“Tulitambua changamoto ya uzalishaji mdogo wa maziwa kutoka kwa ng’ombe wetu wa asili na kuamua kuifanyia kazi. Tulianza kwa kutafuta taarifa kutoka nchi nyingine na hasa nchi wafugaji wakubwa ili kuona jinsi gani wanakabiliana na changamoto kama hii, tuliwashirikisha wataalamu wetu kutoka Serikalini na wadau wengine na hatimae tulipata ushauri wa kitaalamu na kufikia maamuzi ya kuleta ng’ombe hawa kutoka Afrika Kusini,” alisema Alphonce.

Aliongeza kwamba lengo kubwa ni kukabiliana na changamoto ya kiwango kidogo cha maziwa kutoka kwa ng’ombe wetu wa asili kitu kinachopelekea unywaji mdogo wa maziwa kwa wananchi ambapo takwimu zinaonyesha unywaji wa maziwa nchini bado upo chini yaani asilimia 49 tu.

Kwa upande Afisa Mwandamizi ambaye pia ni  Meneja Uhusiano wa mradi huo ng’ombe kutoka Benki ya Wakulima Tanzania Noah Wilson  alisema kwamba Benki ya TADB kwa kuwa inamilikiwa na serikali imejikita katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kuchagiza sekta ya kilimo na ufugaji kwa kushirikiana na wadau wengine zikiwepo sekta binafsi.

“Benki yetu imejikita kuangalia inawezaje kujumuisha wadau wengine katika sekta ya kilimo na kufanya miradi ya pamoja ambayo italeta tija kwa wakulima na wafugaji. Tumeanza na mradi huu wa ngombe wa kisasa ambao umejumuisha wafugaji, vituo vya utafiti, viwanda, wanunuzi, mashirika ya bima na sisi ambao tupo kwenye sekta ya fedha,” alisema Noah.

Aliongeza kwamba katika kuwalinda wafugaji ambao bado wadogo Ng’ombe hao wa mradi wamewekewa bima kutoka Shirika la Bima Tanzania (NIC) kuhakikisha wanakabiliana na changamoto ya kuanguka kiuchumi pindi yapotokea magonjwa au vifo.

“Wakulima wadogo wakipata hasara kwao inakuwa vigumu kuinuka na kuanza tena kwa haraka, kwa kuliangalia hilo tumewapa bima hawa ngo’mbe wa mradi kutoka NIC ili kuwainua tena iwapo watapata hasara. Bima hizo zimewekwa na kwao wenyewe wafugaji si wanyama pekeyao,” aliongeza.

Akiongelea mwitiko wa wakulima Noah alisema kwamba mradi huo umepolelewa vizuri na wafugaji ambapo mpaka sasa wameendelea kupokea maombi kutoka kwa wafugaji ambao bado hawajapatiwa ng’ombe hao. Aidha, wamejipanga kusambaza mradi huo maeneo mengi mengine hapa nchini ili kukidhi uhitaji uliopo.

Baadhi ya wanufaika wa mradi huo wametoa maoni yao na kuishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi huo ambao si tu utawabadilishia ufugaji wa mazoea lakini pia utawainua kiuchumi na zaidi utatunza mazingira kwani ng’ombe hawa wanafugiwa ndani kupewa mahitaji yote kama maji na chakula wakiwa bandani hivyo kuepusha hata migogoro ya wakulima na wafugaji.

“Nina muda mrefu tangu nianze shughuli za ufugaji miaka zaidi ya 20 sasa, ni shughuli nayoipenda sana. Kwa sasa nina kuku wachache lakini zaidi nafuga ng’ombe ambapo nilipokea ng’ombe wa mradi kwa furaha sana kwani nilimtamani kwa muda mrefu. Nategemea kuvuna maziwa mengi pindi ntakapoanza kumkamua lakini pia naiona tofauti ya maumbile ng’ombe huyu ni mkubwa wa umbo zaidi ya wa asili ambao nilizoea kuwafuga”, alisema Helena Shayo, mkazi wa kata ya Mpombo, Kijiji cha Lusanje, Wilayani Busokelo.

Aidha, Helena anatoa rai kwa wakinamama wenzake wa hapo Kijijini na kote nchini kuchangamkia fursa zinazoletwa na serikali kwani Serikali imekuwa ikiwatambua kina mama na kuwaunga mkono kwa mikopo ya aina mbalimbali ikiwemo ya fedha taslimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.