Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Amekutana na Kuzungumza na Ujumbe wa Umoja wa Ulaya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Ujumbe wa Umoja wa Ulaya (EU) walipofika Ofisini kwake Vuga, kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ofisi yake Vuga Wilaya ya Mjini Unguja.

Na.Abdulrahim Khamis.OMPR.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeelekeza nguvu zake katika Uchumi wa Buluu ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo alipokutana na Timu ya Umoja wa Ulaya (EU) walipofika Ofisini kwake Vuga kutaka kujua hali ya Zanzibar na maendeleo yake Chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Mhe. Hemed ameeleza kuwa Sekta ya Uchumi wa Buluu itasaidia kukuza kipato cha Nchi kwa zaidi ya Asilimia 60 hatua ambayo itapelekea Zanzibar kufikia malengo ya maendeleo.

Aidha ameeleza kuwa Sekta ya Uchumi wa Buluu imejumuisha fursa nyingi zikiwemo Utalii,  Uchimbaji wa Mafuta na Gesi pamoja na uvuvi.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa wananchi wa Zanzibar watanufaika kwa kupata fursa za ajira,  kukuza kipato, viwanda pamoja kukuza biashara za ndani na nje ya Nchi.

Kuhusu hali ya Kisiasa Mhe. Hemed amewaeleza kuwa Zanzibar ipo katika hali ya Amani na Utulivu ambapo chini ya miongozo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi ambapo ushirikishwaji wa Vyama vinavyounda Serikali ya umoja wa kitaifa ni wa kuridhisha akitolea mfano Uwakilishaji katika wajumbe wa Baraza la Mapinduzi.

Aidha ameeleza kuwa Serikali ipo tayari kupokea maoni kutoka kwa wadau mbali mbali wa Vyama vya Siasa ambayo yana maslahi na Wazanzibari kwa kuzingatia Sheria na kanuni zilizopo.

Pamoja na mambo mengine Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla  amewaeleza kuwa Serikali imezingatia usawa wa kijinsia katika nafasi mbali mbali za Uongozi ili kuendana na kasi ya Dunia ilivyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri kwa Afrika kwenye Nchi zinazounda Umoja wa Ulaya Bi Yamina Guerfi ameeleza kuwa wamekuja Zanzibar kujua maendeleo na mikakati iliyopo kwa maslahi ya Wananchi.

Aidha amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Umoja wa Ulaya utaendeleza mashirikiano yaliyopo baina yao na Tanzania na kueleza kufurahishwa kwao na muendelezo uliopo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayiundwa kwa mfumo wa Umoja wa Kitaifa akitolea mfano Amani na ulituvu uliopo.

ABDULRAHIM KHAMIS

AFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS

11 JUNI 2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.