Habari za Punde

Mhe. Hemed Amewataka Waumini wa Kiislam Kutumia Misikiti kwa Darsa kwa Rika Mbalimbali ili Kuijua Dini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kuashiria kuufungua Msikiti wa Masjid Jamaa Saif Bin Abdullak Said Almugheri Maungani Wilaya ya Magharibi "B" Unguja, kabla ya Sakla ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid hiyo leo 17-6-2022. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akitoa nasaha zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Masjid Jamaa Saif Bin Abdullah Bin Said Almughery baada ya kuufungua Msikiti huo uliopo Maungani Wilaya ya Magharibi ‘B’

Waumin wa Dini ya Kiislamu wametakiwa kutumia Misikiti katika kuandaa Darsa kwa rika mbali mbali ili Waumini wapate kuijua Dini yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ametoa Kauli hiyo mara baada ya kuufungua Masjid Jamaa Saif Bin Abdullah Bin Said Almughery uliopo Maungani Wilaya ya Magharibi "B" sambamba na kujumuika na Waumini wa Msikiti huyo katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema Mskiti ni Sehemu pekee inayotumika katika kutoa elimu ya Dini ili Waislamu waweze kumjua Mola wao na kujua sheria mbali mbali zilizopo.

Mhe. Hemed amewasisitiza Waumini hao kuandaa Darsa maalum kwa watoto kwa kuandaa Masomo ya Maadili ambayo yatasaidia kuwajenga watoto kiimani na kumjua mola wao jambo ambalo litapelekea kupata kizazi sikivu na chenye maadili.

Alhajj Hemed ameendelea kuwasisitiza Waumini hao kuutumia Mskiti huo kwa mambo yenye kuleta tija ikiwemo kusuluhisha Migogoro mbali mbali iliyomo katika Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuwataka Waumini hao kuhuwisha na kuimarisha Mskiti hasa suala la usafi ili kuweka nidhamu kama Sheria ilivyoelekeza  umuhimu wa suala la usafi katika Uislamu.

‘’Niwaase wanakijiji tuutunze Mskiti huu uzuri huu unahitaji kuendelezwa hii ni sehemu ya Ibada inahitaji kila wakati kuwa safi kama Dini yetu ilivyoeleza kuwa Uislamu ni usafi’’

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Mahmoud Mussa Wadi ameeleza kuwa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar itasimamia upatikanaji wa Viongozi bora watakaosimamia na kuendesha Mskiti huo na kueleza kuwa Ofisi ya Mufti iko tayari kushirikiana na waumini wa Mskiti huo kupata viongozi hao.

Aidha Sheikh Mahmoud amewataka Waumini hao kuepuka Migogoro inayojitokeza baadhi ya Misikiti na kuwataka kuwa wamoja  ili kuendeleza Ibada mbali mbali Msikitini hapo.

Akitoa Khutba ya Ijumaa Ustadh Abdulkarim Said ameeleza kuwa Uislamu umeelekeza suala la kuimarisha Misikiti akitolea Mfano fadhila zinazopatikana kwa yule anaejenga Misikiti.

Aidha Ustadh Abdulkarim ameeleza kuwa Msikiti ni sehemu pekee  inayopendeza mbele ya Allah ambapo ni wajibu wa kila Muumini kuutumia kwa kufanya Ibada mbali mbali zenye kuridhiwa na Allah.

Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

17/06/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.