Habari za Punde

Mpaka Miembe Izae.

 
Na.Adeladius Makwega-DODOMA

Juni 5, 2022 nilitembelewa na rafiki mmoja tuliyempachika jina la utani la Ngosha, ndugu huyu alipofika kwangu tulizungumza mambo mengi sana ya tafakari za uongozi.

Binafsi nilikuwa na kiu ya kufahamu ndugu huyu alifikaje Chamwio Ikulu? Ndugu huyu mchangamfu sana, mwenye matamshi ya Kisukuma alinijibu kuwa yeye ni mzaliwa wa  Kata Kisesa, Wilaya ya Magu, mkoa wa Mwanza na alifika Chamwino Ikulu mapema  sana wakati wa ujenzi wa ukuta wa Ikulu ya Chamwino.

“Tuliambiwa jamani Chamwino Ikulu kuna kazi za ujenzi, tulikuja vijana karibu 80, wakiwamo mafundi ujenzi na vibarua (saidia fundi). Huku mwanzoni tukifanya kazi kadhaa za mikono bila ya kujali kuwa huyu ni fundi na huyu ni kibarua. Kazi hizo zilifanyika hadi Mheshimiwa Magufuli anahamia Dodoma.”

Pia ndugu huyu aliniambia katika kazi hiyo alipata pesa ambazo zilimsaidia mno hadi akanunua maeneo ambayo sasa anayatumia kwa kilimo na makazi yake.“Magufuli kwangu ni kama baba, natambua bila ya yeye nisingepata haya maeneo, mke wa Kigogo na hata Chamwino Ikulu ningekuwa ninaisikia redioni tu.”

Ndugu huyu aliongeza kuwa wakati anaondoka Magu kuja Dodoma yeye alikuwa ni Katibu wa CCM wa kata mojawapo wilayani ya Magu, pia alikuwa ni mwenyekiti wa kamati ya shule mojawapo ya msingi.

“Nafasi ya katibu a CCM wa kata itazibwa katika uchaguzi wa CCM wa ndani ya chama wa mwaka huu, mpaka sasa jina langu linasoma kuwa mimi ni katibu wa CCM wa kata.”

Ndugu huyu anasema kwa desturi ya watu wa Magu na ukanda huo mzima ikiwamo mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Simiyu wana utamaduni mmoja mzuri sana kwa viongozi wapya kuliko maeneo mengi aliyoishi yeye.

Anasema kwao wana miti mingi ya miembe, alipomuuliza babu yake ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa kijiji alimpa siri moja ambayo alikuwa haifahamu juu ya kuwepo kwa miembe mingi.

Anasema kuwa jamiii ikishakubaliana kuwa mwenyekiti wetu ni fulani, hapo kunakuwa hakuna wa kumpinga huyo aliyechaguliwa. Aliyechaguliwa  anaambiwa kuwa sasa wewe umeshakuwa ni kiongozi ili uweze kufanya kazi vizuri unapaswa kupanda miti ya matunda,  miti hiyo unapaswa kuihudimia hadi iwe mkubwa na uzae matunda, hapo ndipo ataruhusiwe kuongea  hadharani na wanakijiji wake na ndipo kazi za uongozi wake zinaanza.

“Mwembe tangu kupandwa hadi kuzaa ni kati ya miaka mitano hadi saba, kipindi hicho chote kiongozi huyu anakuwa kimya, huku akishiriki katika vikao vya kijiji akiwa mbele lakini wanaozungumza ni wazee na wale viongozi wa zamani tu yeye kuongea huwa ni mwiko kwani miembe yake bado haijazaa matunda.”

Kuupanda mwembe siyo shida, kazi ni kuutunza kwa kuwa kwao wana mfugo mingi kama mbuzi, kondoo, ng’ombe na punda ambao ni walaji wa majani.

Ndani ya kipindi chote cha miaka kati mitano na saba kiongozi huyo lazima awe mwanazuoni hodari wa somo la uongozi, namna wazee wanavyofanya kazi, huku mwembe nao ukikua taratibu na pale matunda yakianza kuzaa ndipo mwenyekiti anaweza kuwa na ruhusa ya kuongoza na kuongea hadharani.

Baada ya kuniambia hayo ndugu Ngosha aliondoka zake na mie kubaki zangu kwangu nikitafakari hili la kiongozi mpya na kupanda miembe.

Je wewe mwezetu ni kiongozi? Je umepanda miembe mingapi? Je umeshaanza kuimwagilia ? Au imeshaanza kuzaa ?

Ndugu Ngosha aliniuma sikio kwa kusema kuwa wengi  wetu wanaanza kuongoza na kuongea sana kabla ya kupanda miembe.

Mwanakwetu panda miembe, imwangilie, itunze, isiliwe na mifugo alafu ikizaa ruhusa ya kuongea itatolewa tu, kwa maana miembe inayozaa uliwa na sote lakini pia huwa ni alama ya uongozi wako.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.