Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzin Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ameipongeza Azma ya Timu ya Southampton Kuutangaza Utalii wa Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa jezi namba 10 ya Timu ya Southampton yenye jina lake na Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa Timu hiyo David Thomas, baada ya kumaliza mazungumzo yao yalioyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar  leo 16-6-2022.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa bendera ya Timu ya Southampton na Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa Timu hiyo David Thomas, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar, walipofika kwa mazungumzo na kijitambulisha na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Timu ya Southampton kutoka Nchini Uingereza walipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kijitambulisha (kulia kwa Rais) Mshauri elekezi. Ammy Ninje na Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa Timu hiyo David Thomas,na (kushoto kwa Rais) Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Uongozi wa Timu ya Southampton kutoka Nchini Uingereza ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa Timu hiyo David Thomas, walipofika Ikulu kwa mazumgumzo na kumkabidhi Jezi ya Timu yao, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo 16-6-2022

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza azma ya timu ya Southampton inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza    (EPL) ya kuutangaza utalii wa Zanzibar.                                                                      

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar, wakati alipokutana na uongozi wa timu ya Southampton ukiongozwa na David Thomas ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa timu hiyo wakiwa na wenyeji wao uongozi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale ya Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa sekta ya utalii imekuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa Zanzibar, hivyo hatua hiyo itaimarisha lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kuutangaza utalii wake pamoja na vivutio vilivyopo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa ana matumaini makubwa kwamba azma hiyo ya uongozi wa timu ya Southampton ya kuutangaza utalii wa Zanzibar utazaa matunda kutokana na ligi ya Uingereza kuwa na mashabiki wengi duniani na kuifanya kuwa ni miongoni mwa ligi zinazopendwa ulimwenguni.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa uongozi wa timu hiyo inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza (EPL), kwa kuonesha hamu ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuutangaza utalii wa Zanzibar.

Akizungumza kwa upande wa michezo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na vipaji vya michezo hasa katika mpira wa miguu hivyo, ipo haja ya timu hiyo kuunga mkono azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwepo kwa vituo vya kufundishia michezo hapa nchini.

Hivyo, alisisitiza kwamba hatua hiyo itafungua ukurasa mpya wa michezo hapa Zanzibar na kuweza kuendelea kuibua zaidi vipaji.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa timu ya Southampton David Thomas alieleza azma ya timu hiyo ya kuisaidia Zanzibar katika kuutangaza utalii wake.

Alisema kuwa ana matumaini makubwa kwamba azma hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuutangaza utalii wa Zanzibar hasa kupitia sekta ya michezo.

Alieleza kwamba michezo imechukua nafasi kubwa duniani hivi sasa na imekuwa ikitumika kwa kiasi kikubwa kuitangaza sekta ya utalii hivyo, alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba timu yake ya Southampton itakuwa balozi wa kuutangaza utalii wa Zanzibar ambao umejaaliwa kuwa na vivutio lukuki.

Mapema Mshauri Elekezi wa timu hiyo ya Southampton, Ammy Conrad Ninje alimueleza Rais Dk. Mwinyi lengo la ziara ya viongozi hao hapa Zanzibar inayokwenda sambamba na azma ya timu hiyo ya kuutangaza utalii wa Zanzibar kwa kupitia sekta ya michezo hasa mpira wa miguu.

Nao uongozi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale ulimueleza Rais Dk. Mwinyi hatua zinazoendelea kati ya Wizara hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kukaa pamoja na uongozi huo wa timu ya Southampton  kujadili juu ya mustakabali wa azma  hiyo.

Uongozi huo wa Wizara ya Utalii ulieleza kwamba tayari wanaendelea na vikao na uongozi wa timu hiyo hapa Zanzibar ili kuhakikisha malengo pamoja na azma hiyo inafikiwa kwa kuleta matokeo chanya na kuweza kuitangaza Zanzibar kiutalii duani.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.