Habari za Punde

Serikali Inaifanyia Kazi Changamoto ya Msongamano wa Magari Mpaka wa Tunduma.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali kuhusu geti la Tunduma kuzidiwa katika kutoa huduma lililoulizwa bungeni jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)

Na.Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

Serikali imeahidi kuendelea kutatua changamoto ya msongamano wa magari katika Kituo cha Forodha Tunduma ikiwemo kuangalia uwezekeno wa kuongeza kituo kingine.

Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande alipojibu swali la Mbunge wa Momba, Mhe. Condester Michael Sichwale aliyetakakujua wakati ambao Serikali itaongeza geti jingine ndani ya Jimbo la Momba kutokana na geti la Tunduma kuzidiwa katika kutoa huduma.

Mhe. Chande alisema katika kurahisisha biashara kati ya Tanzania na Zambia na kuondoa changamoto ya msongamano wa magari katika Kituo hicho cha Tunduma, Serikali inaendelea kuchambua na kutathmini taratibu zilizopo ili kuona kama kuna uwezekano wa kuongeza Kituo cha Forodha.

Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuondokana na changamoto ya msongamano wa magari ambapo Januari 2021, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliingia makubaliano na Mamlaka ya Mapato Zambia yanayoelekeza hatua mbalimbali za kuchukua kwa kila nchi”, alisema.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni kuunganisha mfumo wa TANCIS wa TRA na mfumo wa ASCUDA World wa Zambia ili kuiwezesha Idara ya Forodha Zambia kupata taarifa za shehena ya mzigo husika kabla ya kuwasili mpakani, na Serikali ya Zambia kufanya maboresho ya miundombinu ya barabara na eneo la kuegesha magari kupitia ufadhili wa TMEA (Trademark East Africa).

Mhe. Chande alisema pamoja na makubaliano hayo, Serikali kwa upande wa Tanzania ilianzisha Kituo cha Pamoja cha Forodha (One Stop Border Post, OSBP) ambacho kimesaidia taasisi zote za Serikali kuwa sehemu moja na kuwasiliana kwa haraka.

Alisema pia kuwa Serikali kupitia ufadhili wa TMEA imenunua scanners tatu (3) ambazo ni baggage scannerbody scanner na cargo scanner. Aidha, baggage scanner na body scanner zinafanya kazi na cargo scanner inatarajiwa kuanza kufanya kazi mwezi Julai 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.