Habari za Punde

SMZ yaingia mkataba na benki ya NBC kuboresha ukusanyaji wa mapato

Na Kijakazi Abdalla  --  Maelezo Zanzibar.  28/06/2022

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia Wakala wa Serikali Mtandao  imetiliana saini mkataba wa makubaliano(MoU)  na benki ya NBC kwa ajili ya kuboresha ukusanyaji na malipo ya mapato Zanzibar.

Utiaji saini huo ambao kwa upande wa Serikali umetiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa wakala wa Serikali mtandao Said  Seif Said na kwa upande wa Benki ya  NBC umetiwa na Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo Theobald Sabi huko katika ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa ndege.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa wakala wa Serikali Mtandao alisema mkataba huo ni moja ya hatua kubwa iliyofikiwa na   Serikali katika uchumi wa kidigital.

Aidha alisema  Benki ya  NBC itasaidia katika ukusanyaji wa mapato na malipo  kutokana na Serikali ina mfumo wa mapato yote kukusanywa kupitia mtandao wa ZAN Malipo utaweza kufikia malengo kwa haraka .

Amesema Serikali  kwa kushirikiana na Benki ya  NBC itafaidika kupitia mfumo huo kutokana na benki hiyo kuwa  tayari kuboresha miundombinu ya mifumo ya ulipaji ili kuona inafanya kazi kwa ufanisi na haraka.

Vilevile Mkurugenzi  alisema katika kuweka mfumo wa kielektroniki wa makusanyaji mapatoya malipo ya Serikali ya  Zanzibar wakala hao waliopewa dhamana wana dhamira ya kuhakikisha kwamba wanashirikiana na washirika wote wenye uwezo katika kufikia kiwango cha juu kidigitali katika nyanja zote za vituo vya utoaji huduma za umma.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya  NBC, Theobald Sabi alisema ujio wao visiwani humu ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi katika kuchangia ukuaji wa uchumi kwa wananchi  kupitia mifumo ya kimtandao.

Aidha alisema  Benki yake ina nia ya kuzifanya huduma za kibenki ziwe rahisi  na nafuu ili kutoa urahisi unaohitajika kwa wateja wao ..

Vilevile  alisema  Benki hiyo inajitahidi kuendelea na kuwekeza katika suluhisho za kiteknolojia ili kufanya benki kuwa sehemu ya maisha na kutoa suluhu zinazomlenga mteja.

Wakala wa Serikali Mtandao ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kupitia sheria nambari 12 ya mwaka 2019  yenye jukumu la kuratibu,kusimamia na kukuza mipango ya Serikali ya kielektroniki na kutekeleza sera,sheria,kanuni,viwango na miongozo ya taasisi za umma zinazohusiana na Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.