Habari za Punde

WIZARA YA MAMBO YA NJE YAWAPIGA MSASA WABUNGE KUHUSU UMUHIMU WA KUDHIBITI MIGOGORO

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi Fatma Rajab akifungua mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama yaliyofanyika leo tarehe 4 Juni 2022 Bungeni, jijini Dodoma.

Serikali ya Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa jitihada za kuleta amani barani Afrika hususan eneo la ukanda wa maziwa makuu, kupitia ushiriki wake katika kutatua migogoro na kuchangia vikosi vya kulinda amani.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Mohammed Rajab alipozungumza leo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa warsha kuhusu Utatuzi wa Migogoro iliyotolewa na Wizara kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa lengo la kuwajengea uwezo.

Amesema kuwa, kwa miaka mingi Tanzania imeendeelea kushirikishwa kwenye utatuzi wa migogoro na kuchangia vikosi vya kulinda amani kutokana na kuaminika kwake kikanda na kimataifa kwenye eneo hilo na hii inatokana  na hali ya amani na utulivu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii iliyopo nchini.

“Jukumu la Wizara ni kusimamia uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbalimbali na mashirika ya kikanda na kimataifa kwa lengo la kulinda maslahi ya nchi. Ni kutokana na kutekeleza jukumu hilo, Tanzania imeendelea kuaminika na kushirikishwa katika utatuzi wa migogoro mbalimbali Afrika. Hiki ni kielelezo cha kuaminika”, amesema Balozi Rajab.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa amesema kuwa viongozi wakiwemo Wabunge wanayo nafasi kubwa katika kuchangia amani kupitia nafasi zao kwa kutoa elimu ya uzalendo kwa wananchi kwa kuwaelimisha kutojiingiza kwenye masuala yanaweza kusababisha migogoro na uvunjifu wa amani ndani ya jamii.

“Kila mmoja wetu atumie nafasi yake kuzuia migogoro katika jamii ikiwemo ile inayosababishwa na siasa. Wizara iendelee kutoa semina hizi na Kamati itaendelea kutoa ushirikiano na ushauri unaohitajika kwa Wizara”, alisisitiza Mhe. Kawawa.

Akiwasilisha mada kuhusu “Utatuzi, Udhibiti na Usuluhishi wa Migogoro” Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia cha jijini Dar es Salaam, Dkt. Ally Masabo amesema ujenzi wa imani na kujiamini kwa wananchi na siasa safi ni njia mojawapo ya kudhibiti migogoro ndani ya jamii. Pia ameongeza kuwa, Tanzania ipo mstari wa mbele katika utatuzi wa migogoro na uchangiaji wa vikosi vya ulinzi wa amani kutokana na ukweli kwamba eneo lote linaloizunguka Tanzania likiwa salama nchi inanufaika zaidi.

“Tanzania ni nchi ya 13 ulimwenguni katika kuchangia walinzi wa amani na ya sita Afrika. Hii inatokana na imani ya Tanzania kwamba amani ni chanzo cha maendeleo. Tanzania inaamini kwamba nchi zinazotuzunguka zikiwa salama nchi inanufaika kuliko zikiwa katika migogoro” amesema Dkt. Masabo.

Wakichangia mada hiyo, Wajumbe hao wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wamepongeza utaratibu wa Wizara wa kutoa semina za aina hiyo kwao na kuongeza kuwa, ipo haja kwa Serikali kuwa na Program za uelimishaji umma kuanzia ngazi za chini kuhusu umuhimu wa amani na madhara yanayotokana na migogoro katika jamii.

Pia wamesisitiza elimu ya kuwawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kwa kufanya kazi na kujishughulisha itolewe kwa wingi ili kuepuka migogoro inayosababishwa na wananchi kutojishughulisha na kusubiri Serikali iwanyie kila kitu.

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi Fatma Rajab akifungua mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama yaliyofanyika leo tarehe 4 Juni 2022 Bungeni, jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vita Kawawa akifafanua jambo wakati wa majadiliano kwenye mafunzo hayo.

Mkurugenzi wa Idara wa Siasa, Ulinzi na Usalama katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi akitoa neno la shukurani kwa jumbe wa kamati hiyo.
Mhe. Cosato Chumi akichangia hoja wakati wa majadiliano, kulia ni  Mhe. Janeth Masaburi akifatilia mafunzo.

Sehemu ya Wajumbe wa kati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, kutoka kushoto ni Mhe. Bonnah Kamol na Mhe. Fakharia Shomar Khamis wakifuatilia uwasilishaji wa mada ya migogoro.
Mhe. Abeid Ramadhani akichangia hoja wakati wa majadiliano kwenye mafunzo hayo.

Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia, Dkt. Ally Masabo akiwasilisha mada ua udhibiti wa migogoro kwa kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mafunzo yakiendelea, wa kwanza kulia ni Mhe. Stella Ikupa akifuatilia majadiliano.


Mhe. Zahor Mohamed Haji akifafanua juu ya umuhimu wa mafunzo hayo kwa Waheshimiwa Wabunge na umuhimu wa kulinda kauli zao ili kuepuka kuwa vyanzo vya migogoro katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Felista Njau akieleza umuhimu wa Wabunge kutambua matatizo ya msingi katika jamii wanazoziwakilisha na kuyatatua kwa wakati ili kuepuka kuzuka kwa  migogoro na kuathiri amani ya Taifa.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasiliamali Watu, Bw. Alex Mfungo akichangia jambo wakati wa majadiliano kwenye mafunzo hayo.
Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Diplomasia, Bw. Felix Wandwe na Mkurugenzi wa Idara ya Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caroline Chipeta wakifuatitilia mafunzo.

Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifatilia mafunzo.
Sehemu nyingine ya Maafisa wa Wizara ya Mambo ya nje wakifuatilia mafunzo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.