Habari za Punde

Lugha ya Kiswahili ni Daraja Linalowaunganisha na Kuwaweka Pamoja Wana Jumuiya Afrika Mashariki.-Dk. Mwinyi

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B” Unguja leo 7-7-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la   Mapinduzi  Dk. Hussein Mwinyi  amesema lugha ya Kiwahili ni daraja linalowaunganisha na kuwaweka pamoja wana Jumuiya Afrika Mashariki.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, hafla iliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, iliopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Jijini Zanzibar.

Alieleza kuwa  lugha ni nyenzo muhimu kwa utangamano na kusema  lugha ya Kiswahili imekuwa ikitumika kama daraja la kuwaunganisha na kuwaweka pamoja wana Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akinasibisha maelezo hayo  na Kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo ‘Kiswahili kwa amani, ustawi na Utangamano wa kikanda’ ; Dk. Mwinyi alisema Historia inabainisha kuwa maendeleo ya ukuaji na kuimarika kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili kumechangiwa na mambo kadhaa ikiwemo shughuli za biashara kupitia misafara ya nchi kavu na baharini baina ya watu wa mwambao wa Afrika Mashariki.

Alisema kufanyika kwa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani kwa mara ya kwanza hapa Zanzibar kumeendelea kuijenga Historia ya lugha hiyo na kuiongezea heshima Zanzibar katika juhudi zake za kuiendeleza lugha ya Kiswahili Duniani.

“Hapana shaka hatua ya kukipa Kiswahili hadhi ya kuwa na siku yake maalum si jambo dogo  na ni heshima kubwa iliopewa lugha hii”, alisema.

Alisema ni jambo la faraja  na kutia moyo kuona juhudi mbali mbali zinaendelea kufanywa an nchi za Jumuiya Afrika Mashariki katika kukiendeleza, kukienzi na kukitukuza Kiswahili.

Rais Dk,. Mwinyi alisema Mkutano wa kikao cha 21 cha Viongozi wa Afrika  Mashariki kilichofanyika  February 2021  uliiidhinisha  Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (kikazi)katika mikutano ya kimataifa kama vile, Mikitano ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na mikutano ya Umoja wa Afrika (AU).

Alitumia fursa hiyo kuzitaka nchi zote  kuona umuhimu na kuitumia fursa hiyo ya kutangamana kwa kukubali kutumia wataalamu wa kiswahili kwa njai ya kubadilishana au kuajiri katika shughuli mbali mbali.

Alisema namna bora ya kufurahia uamuzi wa kuwa na Siku ya Kiswahili Duniani ni kuongeza juhudi katika kuimarisha lugha hiyo katika Jumuiya Afrika Mashariki  pamoja na taasisi mbali mbali ili kukuza Kiswahili kwa kuzingatia wajibu walionao katika  kubuni mbinu bora za kuendeleza lugha hiyo.

“Sisi wenyewe kwanza tuna wajibu wa kuonyesha mapenzi kwa lugha yetu kwa kuizungumza kwa ufasaha na usahihi ili tuwe walimu wazuri kwa wanaojifunza”, alisema.

Alisema kuendlea kukua kwa Kiswahili kumeongeza mahitaji ya wataalamu wa lugha hiyo Duniani kupitia nyanja mbali mbali, ikiwemo walimu, waandishi wa vitabu, wakalimali na watangazaji wa vyombo vya habari.

Alisitiza umuhimu wa taasisi mbali mbali za elimu kuona mahitaji yanayongezeka ya lugha hiyo na kutumia ipasavyo  fursa hiyo kama bidhaa inayoweza kuzalisha ajira.

Alieleza kuwa Serikali ya Jamuhuri ya Muuungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuunga mkono Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki katika juhudi za kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili.

Aidha, aliwapongeza wale wote waliobuni jambo hilo, wakiwemo wadau mbali mbali wa kiswahili na hususan Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Mapema, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale katika hotuba yake iliosomwa   na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Simai Mohamed  Said alisema uamuzi wa  maadhimisho hayo kufanyika kwa mara ya kwanza hapa Zanzibar ni jambo la busara na yamezingatia kuwa Zanzibar ndio Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili  Afrika Mashariki sambamba  na kuwa kitovu cha lugha hiyo.

Alieleza matumaini yake kuwa taaluma iliyopatikana katika Kongamano la Lugha ya Kiswahili lililofanyika jana itatoa mchango muhimu katika dhamira ya Kamisheni ya Kiswahili Afrika mashariki ya kuiendeleza lugha hiyo.

Alitoa rai kwa Nchi za Jumuiya Afrika Mashariki  kutumia fursa ya kupata walimu wa lugha ya kiswahili kutoka Zanzibar, kw akigezo kuwa kuna walimu w akutosha na wenye uwezo w akufundisha lugha hiyo, huku nayo ikiwa na mahitaji ya kupata walimu wa masomo ya Sayansi na Hesabati. 

Nae, Naibu Katibu Mkuu Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhandisi Steven Mlote alisema lugha ya kiswahili ina umuhimu mkubwa katika utangamano wa Jumuiya Afrika Mashariki, ikiwa na nafasi kubwa katika kujenga na kuimarisha amani katika nchi mbali mbali za Jumuiya Afrika Mashariki.

Alisema kauli mbiu ya  maadhimishi hayo inayosema  “kiswahili kwa amani, Ustawi na Utangamano wa Kikanda”  inakidhi malengo ya Jumuiya hiyo katika jitihada zake  za kukuza utangamano wa kikanda.

Alieleza kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina bahati  kubwa ya kuzungumza lugha hiyo ambayo haikurithiwa na wakoloni na ikiwa na matumizi mapana Duniani.

Aidha, kwa nyakati tofauti wakitoa salamu za nchi zao,  Wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya Afrika Mashariki kutoka Burundi, Kenya,Rwanda, Sudan Kusini na Uganda walipongeza juhudi za Jumuiya Afrika Mashariki na Kamisheni ya  Kiswahili ya Afrika Mashariki ya kufanikisha vyema maadhimisho hayo.

Wawakilishi hao alisema kufanyika kwa maadhimisho hayo hapa Zanzibar kwa mara ya kwanza ni historia ya pekee katika kukuza lugha hiyo na kubainisha kuwa Kiswahili ni lugha ya kwanza Afrika na ya nane Duniani kwa kuwa na siku maalum ya kuadhimishwa.

Walisema wamepokea na kuthamini tamko la Shirika la  Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) la kuitambua Julai 7 kuwa siku ya Kiswahili Duniani, wakibainisha kutumika kwa ajili ya kujenga amani na ushirikiano.

Wawakilishi hao  walisema Kiswahili ni lugha ya nne nchini Rwanda ambapo hufundishwa katiika skuli zote, ambapo pamoja na mambo mengine kinalenga kudumisha ujirani mwema.

“Tunahitaji misaada kutoka nje ya nchi yetu ili kupata msukumo wa matumizi ya lugha ya kiswahili......lugha hii itaweza kuiunganisha jamii”, alisema.

 John Ayem Mareech kutoka Suda Kusini.  

Katika hatua nyengine, Katibu Mtendaji wa Baraza la kiswahili Zanzibar (bakia) Dk. Mwanahija Juma alitumia fursa hiyo kusisistiza nchi za Jumuiya Afrika Mashariki kaunzisha Mabaraza ya kiswahili ikiwa ni hatua thabiti ya kuiendeleza lugha hiyo.

Aidha, akimuwakilisha Katibu mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Mchunguzi Lugha Mkuu wa BAKITA Dk. Rizati Mmari  alisema ni muda muafaka kwa nchi zisizo na mabaraza ;kuanzisha kwa kigezo kuwa ni muhimu ambapo miongoni mwa shughuli zake muhimu ni kutoa mafunzo ya vitendo kwa wakalimali na wadau wengineo.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Kitaifa akiwemo Mama Mariam Mwinyi,  Viongozi wa Jumuiya Afrika Mashariki, Kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki pamoja na wadau mbali mbali wa lugha ya Kiswahili nchini.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.