Habari za Punde

Uwekezaji Sekta ya Uvuvi.

Na.Mwandishi Wetu.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatamah amekutana na Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Multi Marinetime kutoka Norway, Bw. Gustav Nydal kwa lengo la kujadiliana namna wanavyoweza kushirikiana katika uwekezaji ili kuendeleza sekta ya uvuvi.

Dkt. Tamatamah amesema kuwa majadiliano hayo yamekuja wakati muafaka kwa sababu serikali sasa ipo katika mchakato wa kujaribu kufungamanisha sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu ikiwemo kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi kutoka baharini.

Amesema kwa upande wa bahari wapo katika mchakato wa ununuzi wa meli nane na tayari wameshakutana na makampuni mbalimbali ya utengenezaji wa meli ikiwemo hiyo ya Multi Maritime ili kuona kampuni itakayofaa kwa ajili ya kutengeneza meli hizo.

Aliongeza kuwa katika bajeti ijayo ya mwaka 2022/2023 sekta ya uvuvi imepewa bilioni 60 na kati ya hizo bilioni 11 zitatumika kununua boti kwa ajili ya wavuvi wadogowadogo hivyo wanaangalia uwezekano wa serikali kushirikiana na kampuni hiyo ili ikiwezekana kampuni hiyo itengeneze boti hizo.

Naye Mwakilishi wa Kampuni Multi Marinetime kutoka Norway, Bw. Gustav Nydal amesema nia yao ni kushirikiana na Tanzania katika kutengeneza meli na boti za kisasa za ukubwa wa kati ili ziweze kurahisisha shughuli za uvuvi kwenye ukanda wa pwani ya bahari.

Multi Maritime ni Kampuni ya Kimataifa kutoka Norway inayojiashughulisha na utengenezaji wa meli kubwa na boti za uvuvi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.