Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amezitaka Wizara za Habari za SMT na SMZ kuvitumia Vyombo vya Habari katika kuelimisha Jamii kujua Mfano wa Masuala ya Msingi watakayoulizwa katika Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ifikapo Agosti 23 Mwaka huu.
Mhe. Majaliwa ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Kitaifa Sensa ya watu na Makazi 2022 ameyasema hayo katika Kikao cha Sita cha Kamati hiyo kilichofanyika Ukumbi wa Melia Hotel Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema ili kuwaweka tayari Wananchi kukabiliana na Zoezi hilo ni vyema kuwa na ufahamu mapema namna atakavyohojiwa ili kurahisisha na kuondoa hofu kwa Wananchi.
Mhe. Majaliwa amesema Jamii ya Watanzania inafatilia zaidi Mitandao ya Kijamii hivyo ni vyema kutumia Fursa hiyo kwa kuelekeza nguvu ili kurahisisha Zoezi hilo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameeleza kuwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Sekretarieti ni zenye kuthaminiwa ambapo ameipongeza kwa mashirikiano mazuri waliyokuwa nayo kwa pande zote Mbili za Muungano.
Aidha Mhe. Majaliwa amemshukuru Muwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) Nchini Tanzania kwa kuendelea kuunga Mkono kwenye uratibu wa Zoezi hilo na kumuhakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwa nao hadi kukamilika kwa zoezi hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Kamati hiyo Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewashukuru Viongozi wa Kitaifa kwa kuonesha Mfano wa Kushajihisha umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi hasa kupitia Ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuwafikia Wananchi wa Mikoa yote ya Zanzibar.
Aidha amewataka Viongozi wote wa Serikali kuendelea kuhamasisha na kueleza umuhimu wa Zoezi hilo na kupongeza Kampeni ya Viongozi mbali mbali kueneza Vipeperushi kupitia Mitandao ya Kijamii inayoonesha utayari wao wa kushiriki katika zoezi hilo.
Samba na hayo Mhe. Hemed ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amezishukuru Taasisi za Kidini na makundi mbali mbali kwa kuendelea kutumia Fursa walizonazo katika kuwahamasisha walio kwenye dhamana zao.
Kwa Upande wao Watakwimu Wakuu wa SMT na SMZ wameeleza kuwa Zoezi la kupata Makarani na wasimamizi wa Sensa limekwisha kamilika ambapo hatua inayoendelea sasa ni kukamilisha Mafunzo kwa Makarani kutoka katika Shehia na Kata.
Wameeleza kuwa Mafunzo wanayopatiwa Watendaji hao ni kuhakikishaZoezi la Sensa ya Watu na Makazi linafanikiwa na kuwataka washiriki kuwa makini kipindi cha Mafunzo ili kufaulu vyema Mitihani na hatimae kufanikisha vyema Zoezi hilo.
Abdulrahim Khamis
Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
30/07/2022
No comments:
Post a Comment