Habari za Punde

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MKUTANO WA SKAUTI WA KIKE AFRIKA TAREHE 22 AGOSTI

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akivishwa Skafu na watoto wa Jumuiya ya Skauti wa Kike Tanzania (Tanzania Girl Guides) mara alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kufungua Mkutano wa 13 wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya za Skauti wa kike(Girl Guides) leo tarehe 22 Agosti 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewaasa wazazi wote katika nchi za Afrika kujitahidi kufuatilia maendeleo ya Watoto shuleni pamoja na kuzungumza nao ili kuweza kutatua changamoto wanazopitia na kuwasaidia kutumia maarifa, ujuzi na vipaji walivyonavyo kwa maendeleo ya bara la Afrika.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika  Ufunguzi wa Mkutano wa 13 wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya za Skauti wa Kike (Girl Guides) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Pia amewasihi viongozi wa dini pamoja na wale wa kimila kushirikiana na serikali katika kulea watoto kimaadili ili kuepusha vitendo viovu na visivyopendeza katika jamii.

Aidha Makamu wa Rais amesema kuporomoka kwa maadili ni jambo lenye athari mbaya katika nchi za Afrika ambalo linachangia kurudisha nyuma jitihada za maendeleo na kuondoa umasikini barani Afrika. Amesema Jumuiya hizo katika mataifa zinapaswa kushirikiana na serikali zao pamoja na wazazi husasani wakati huu wa utandawazi ili kuepusha vitendo vya mmomonyoko wa maadili.

Makamu wa Rais amezipongeza Jumuiya za “Girl Guides” barani Afrika kwa kuendelea kutetea haki za watoto wa kike na wanawake kwa ujumla, kuwajengea uwezo wa kujiamini pamoja na kutengeza viongozi wenye maadili mema waliochangia kuleta maendeleo barani Afrika. Amesema jamii inapaswa kuunga mkono kazi nzuri inayofanywa na jumuiya hizo ya kulea watoto katika maadili nidhamu na kumcha mungu.

Amesema serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa malezi bora na ustawi wa mtoto wa kike na wanawake kwa ujumla, hivyo inaendelea kutekeleza sera ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita kunatoa fursa sawa ya watoto wa kike na kiume kupata elimu. Amesema Tanzania inaendelea kuongeza uwekezaji katika program za elimu kwa ajili ya wasichana, mafunzo ya ufundi stadi na matumizi ya teknolojia, kumkwamua msichana na mwanamke kiuchumi kwa kuhakikisha wanashirikishwa katika maamuzi kupitia uongozi katika nyadhifa mbalimbali.

Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Doroth Gwajima amesema Wizara inaendelea katika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa programu ya kimkakati ambayo ni ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ambayo imelenga kumkuza mtoto katika Nyanja zote muhimu kama vile afya bora, lishe bora, ujifunzaji wa awali pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto. Ameongeza kwamba kwa kushirikiana na wadau wengine tayari wizara inatekeleza ajenda ya taifa ya kuwekeza katika afya na maendeleo kwa vijana balehe kuanzia umri wa miaka 10 - 18 ambayo inalenga kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi, kutokomeza mimba za utotoni, kuondoa ukatili na kuimarisha stadi za Maisha.

Awali Kamishna wa Jumuiya ya Skauti wa Kike nchini Tanzania (Tanzania Girl Guides Association) Bi. Mary Richard amesema Jumuiya hiyo imeendelea kusimamia ustawi wa mabinti na wanawake kwa ujumla kwa kuwapa mafunzo yaliyo nje ya mfumo rasmi wa elimu yanayopelekea binti kujithamini , kujitambua , kujiamini pamoja na kuwa rasilimali kwa taifa.

Ameongeza kwamba Jumuiya hiyo inaendesha shughuli mbalimbali za kutoa elimu ya utunzaji mazingira, elimu ya lishe bora, elimu ya kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya pombe pamoja na kuendesha kampeni za wasichana kuingia kwenye taaluma za sayansi na kupinga ndoa na mimba za utotoni.

Mkutano wa Jumuiya za  Skauti wa Kike (Girl Guides) kanda ya Afrika ni mkutano wa kikatiba ambao hufanyika kila baada ya miaka mitatu. Mkutano huo unafanyika Tanzania tarehe 22 hadi 26 Agosti 2022 ukiwakutanisha wajumbe wa taasisi za guiding kutoka nchi 33 za bara la Afrika ukiwa na kauli mbiu ya “Tustawi Pamoja”.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali baada ya kuwasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kufungua Mkutano wa 13 wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya za Skauti wa Kike (Girl Guides) leo tarehe 22 Agosti 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza  na viongozi , wawakilishi wa mataifa mbalimbali ya afrika pamoja na skauti wa kike nchini Tanzania wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 13 wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya za Skauti wa Kike (Girl Guides) unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Skauti wa Kike kutoka Tanzania Girl Guides Association mara baada ya kufungua Mkutano wa 13 wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya za Skauti wa kike unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Skauti wa Kike kutoka Tanzania Girl Guides Association mara baada ya kufungua Mkutano wa 13 wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya za Skauti wa kike unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Skauti wa Kike kutoka Tanzania Girl Guides Association mara baada ya kufungua Mkutano wa 13 wa Kanda ya Afrika wa Jumuiya za Skauti wa kike unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.