Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi awataka wananchi kuwa wavumilivu ujenzi wa barabara za mjini utakapoanza

Huo ndio muonakano wa Barabara ya Juu (Flyover) itakayojengwa katika maeneo ya Mwanakwerekwe  na Amani Unguja katika Mradi wa Ujenzi wa Barabara katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, leo 6-8-2022 utiaji wa saini ya Ujenzi wa Mradi huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza baada ya kumalizika kwa utiaji wa saini ya Mradi wa Ujenzi wa Barabara za Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja na barabara ya Juu (Flyover) ujenzi huo utakaofanywa na Kampuni ya CCECC kutoka Nchini China.hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kuwa wavumilivu na kustahimili changamoto mbali mbali zitakazojitokeza wakati mradi mkubwa wa ujenzi wa Barabara za Mjini utakapoanza.

Dk. Mwinyi ametoa wito huo Ikulu Zanzibar, baada kukamilika hafla ya utiaji saini ya mradi wa ujenzi wa Barabara za Mjini, unaotarajiwa kutekelezwa na Serikali  hivi karibuni kupitia Kampuni ya China Civil Engeneering Construction Cooperation (CCECC) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Watu wa  China.

Amesema kuna umuhimu wa wananachi kuwa wastahalivu wakati mradi huo utakapoanza kutekelezwa kwa kuzingatia kuwa kazi za ujenzi zitaingilia shughuli za wananchi na wakati mwengine kuibua msongamano barabarani.

Kufuatia hali hiyo, Dk. Mwinyi alivitaka vyombo vya habari nchini kote kuchukua nafasi yao na kuielimisha jamii juu ya kuanza kwa mradi huo mkubwa na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wake.

Aliutaka uongozi wa Mkoa Mjini kuanza kuzungumza na wananchi ili waelewe mazingira yatakavyokuwa wakati kazi za ujenzi zikiendelea na kubainisha matumaini yake ya kuwa na Zanzibar mpya pale  ujenzi huo utakapokamilika.

Alisema mkataba  wa ujenzi wa barabara hizo unalenga kuubadili Mji wa Zanzibar hivyo akazitaka Idara ya Manispaa kuhakikisha inajianda kuweka sheria ndogo ndogo kuhusiana na utunzaji wa barabara hususan katika eneo la hifadhi ya barabara.

“Itakuwa haina maana kutumia fedha zote hizo halafu ukute mtu anafanya biashara  katika eneo la hifadhi ya barabara” alisema.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa hakuna nchi yoyote Duniani ilioweza kupata maendeleo bila ya kuwa na miundo mbinu bora, hivyo akasema hiyo ndio sababu ilioifanya Serikali kuweka kipaumbele katika suala la uimarishaji wa miundombinu ya barabara Mjini na Vijijini.

Alisema kipaumbele hicho pia kinahusu maeneo mengine, ikiwemo uimarishaji wa Viwanja vya Ndege Unguja na Pemba, Bandari ya Malindi na bandari nyenginezo, uwepo wa umeme wa uhakika pamoja na matumizi ya ICT kwa kuzingatia kuwa uchumi wa kisasa unafanyika Kidigitali.

Rais Dk. Mwinyi alisema Uongozi wa Serikali ya Awamu ya nane tayari umekamilisha mikataba ya ujenzi wa barabara za Mijini pamoja na ujenzi wa  Barabara  za Vijijini zenye urefu wa kilomita 200 na akatumia fursa hiyo kuiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kuhakikisha barabara hizo  zinakamilika ifikapo mwaka 2025, huku akitaka Wizara Fedha na Mipango kuhakikisha inafanya juhudi za kupata fedha.

Nae, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Mohamed Salim alisema tukio la utiaji saini ujenzi wa barabara  za Mjini ni muendelezo wa juhudi za Serikali katika kuimarisha miundo mbinu ya kiuchumi hapa nchini.

Alisema ukuaji wa uchumi unategemea uwepo wa miundo mbinu bora ya barabara, ambapo hutoa haiba nzuri kwa watumaji na wageni watakaotemebelea hapa nchini.

Alisema barabara nyingi ziliopo Mjini zilijengwa karibu miaka 50 iliyopita, ambapo mbali na kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara zimekuwa zikiharibika  hususan wakati wa kipindi cha mvua kubwa na kuilazimu Serikali kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 15 kwa matengenzo.

“............... hivyo hatua hii itaondoa matumzii makubwa ya fedha za serikali, itaondoa msongamano, kupunguza ajali barabarani  pamoja na kuleta haiba nzuri ya mji wetu’, alisema.

Aliishukuru Serikali kwa juhudi kubwa ilizochukua na kufanikiwa kupata fedha za ujenzi huo , na akatumia fursa hiyo kumshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Mwinyi Talib Haji pamoja  na Mwanasheria wa Wizara hiyo kwa kupitia vyema mikataba ya ujenzi huo.

Mapema, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya CCECC Zhang Junle akiwasilisha ‘Dhana ya Mradi’ huo alisema utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara za Mjini utadumu kwa kipindi cha miaka mitatu, ambapo barabara zenye urefu wa kilomita 100.94 zitajengwa na kuigharimu Serikali kiasi cha  Dola za Marekani Milioni 116.1 hadi kukamilika kwake.

Alisema pamoja na mambo mbali mbali, mradi utahusisha ujenzi wa barabara za juu ‘Flyover’ katika eneo la makutano Amani pamoja na Mwanakwereke.

Alisema wakati wa utekelezaji wa mradi huo wastani wa wananchi 1000 watapata ajira na kusema  Kampuni hiyo itakuwa na mashirikiano ya karibu na  Serikali pamoja na wananchi.

Junle alisema Kampuni ya CCECC ni Kampuni kubwa iliyotekeleza miradi mbali mbali mikubwa Barani Afrika na kwengineko Duniani, ikihusisha miradi ya ujenzi wa barabara, njia za Reli, mbiundombinu ya usambazaji maji, ujenzi wa daraja pamoja na nyumba za makaazi.

Aidha, alisema hapa Zanzibar ilitekeleza miradi kadhaa ya barabara, ikiwemo barabara ya Bububu- Mahonda- Mkokotoni, Fuoni – Kombeni,Matemwe – Muyuni pamoja na barabara ya Pale – Kiongele, ambapo kw aujumla zina urefu wa  kilomita 54.

Katika hafla hiyo ya Utiaji saini ya Mkataba wa ujenzi wa Barabara za Mjini, Katibu Mkuu Wizara ya ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi  Khadija Khamis Rajab alitia saini kwa niaba ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wakati ambapo Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya CCECC Zhang Junle alitia saini kwa niaba ya Kampuni hiyo.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.