Habari za Punde

SHAKA ATUMIA KIJIWE CHA KAHAWA TABORA KUELEZA MWELEKEO WA RAIS KATIKA KILIMO

 

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa, (NEC) ya CCM, tikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ametembelea kijiwe cha Kahawa Lumumba kilichopo Tabora Mjini na kunywa kahawa na wananchi na kutumia fursa hiyo kuelezea hatua zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuimarisha sekta ya kilimo.

Akiwa kijiweni hapo, Shaka alitoa nafasi ya kusikiliza wananchi hao ambao walitoa pongezi kwa Rais @samia_suluhu_hassan  na Chama Cha Mapinduzi kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuleta maendeleo na kusimamia utekelezaji wa Ilani.

Aidha, wananchi hao walimuombia Shaka kufikisha salamu zao kwa Rais Samia wakimuomba aendelee kuongeza fedha katika sekta ya kilimo ambayo Watanzania wengi wanakitumia kama shughuli rasmi ya kujipatia kipato.

Pia, waliomba kupunguzwa kwa gharama ya maji ambayo wameeleza ni kubwa mjini Tabora.

Akizungumza Shaka ameelezea hatua kwa hatua kuhusu mipango inayoendelea kutekelezwa na serikali ya Rais Samia kuhakikisha maendeleo yanafika maeneo yote huku akieleza pia kuhusu juhudi za kuboresha kilimo.

“Rais Samia kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo ameendelea kuchukua hatua mbalimbali na miongoni mwa hatua hizo ni kuongeza fedha katika bajeti ya kilimo kutoka Sh. bilioni 254 hadi sh. bilioni 999. Ni ongezeko kubwa na ataendelea kuongeza kidogo kidogo hadi mambo yatakuwa sawa,” alisema.

Kuhusu changamoto ya bei kubwa ya ulipaji maji kwa wananchi wa Tabora Mjini, Shaka amesema atalifikisha suala hilo kwa Waziri wa Maji Jumma Aweso kuona hatua gani zinaweza kuchukuliwa kupunguza bei ya maji kama ambavyo wananchi wanaona.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.