Habari za Punde

Wazee CCM wampongeza Rais Mwinyi

 NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

BARAZA la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi(CCM)Zanzibar, wamempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, kwa ziara yake ya kikazi aliyoifanya nchini kuwa imekuwa chachu ya kuimarisha maendeleo endelevu katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bazara hilo, Khadija Jabir wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari huko Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, alisema Baraza hilo na Wana CCM kwa ujumla wanajivunia kuwa na Rais mchapakazi,mfuatiliaji na mwenye maono ya kuleta mageuzi ya kimaendeleo nchini.

Alieleza kuwa kiongozi huyo kupitia ziara hiyo amefanya kazi kubwa ya kukagua,kufungua na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo  na ya kimkakati ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.

“Tunampongeza Rais wetu Dk.Hussein Ali Mwinyi kwa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo nchini nzima katika sekta mbalimbali zikiwemo za miundombinu,elimu,afya na vikundi vya ujasiriamali na kutoa maelekezo ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Tumeona taswira halisi ya hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa chini ya uongozi wake wa awamu ya nane, hivyo tunawashauri viongozi na watendaji wengine waendelee kufanya kazi kwa bidii.”, alisema Mwenyekiti huyo Khadija.

Alisema, ziara aliyoifanya Dk. Mwinyi ilikuwa ya kishujaa ambapo alipanda milima na mabonde Visiwani Unguja na Pemba kuonana na wananchi na kukagua utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati alipopeperusha bendeya ya CCM kuomba kura za wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi 2020.

Katika maelezo yake Khadija, alielezea kuridhishwa kwake na kasi ya utendaji wa Rais kwa kukiri kuwa fedha za ahueni ya uviko 19 inatumika vizuri kuwakomboa kiuchumi wananchi.

Hata hivyo alisema wengine walikuwa hawajui yanayotendeka mikoni, wilayani, majimboni na vijijini lakini baada ya kufuatilia ziara ya Dk. Mwinyi wengi wameona maendeleo makubwa yaliyofikiwa ndani ya muda mfupi wa uongozi wa Dk. Mwinyi.

Alisema, miradi mbali mbali inaendelezwa, mengine ikiwa imekamilika na wakati huo huo mipya imeanzishwa na kuwafaidisha wananchi.

Aidha alisema, wananchi wanafaidika na matunda ya mapinduzi kama inavyoonekana ambapo wananchi wanafarijika sana na uongozi wake wenye neema na faraja.

Alisema, miradi mikubwa ya kimkakati itakapo kamilika, Mapinduzi ya Zanzibar yatazidi kunawiri na uchumi utazidi kuimarika zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.