Habari za Punde

Japan Kununua Kilo Milioni 30 za Tumbaku Tanzania

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na Rais na Mtendaji Mkuu wa JTI, Bw. Masamichi Terabatake, kwenye kikao kilichofanyika katika ofisi za Japan Tobacco International (JTI) zilizopo Kamiacho, jijini Tokyo Japan, Septemba 26.2022. Kutoka kushoto ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Bw. Takashi Araki, Mwenyekiti wa Bodi ya JTI, Bw. Mutsuo Iwai.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi aliyoambatana nao na viongozi wa Japan Tobacco International (JTI) , baada ya kikao kilichofanyika katika ofisi hiyo, iliyopo Kamiacho, jijini Tokyo Japan
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais na Mtendaji Mkuu wa Japan Tobacco International (JTI) Bw. Masamichi Terabatake, baada ya kikao chao kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi hiyo, iliyopo Kamiacho, jijini Tokyo Japan, Septemba 26.2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

KAMPUNI ya Japan Tobacco Incorporation (JTI) imeahidi kununua kilo milioni 30 za tumbaku kutoka kwa wakulima wa Tanzania katika msimu ujao wa kilimo.

 

Ahadi hiyo imetolewa leo (Jumatatu, Septemba 26, 2022) na Rais na Mtendaji Mkuu wa JTI, Bw. Masamichi Terabatake mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyetembelea ofisi zao ili kuwahakikishia utekelezaji wa mazungumzo yaliyofanyika wakati wa mkutano wa TICAD 8, jijini Tunis, Agosti, mwaka huu.

 

Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu amesema uamuzi wa kampuni hiyo kuongeza kiwango cha ununuzi wa tumbaku utatoa ahueni kwa wakulima wa Tanzania ambao walikuwa hawana uhakika wa soko la zao hilo.

 

“Leo Bodi ya Wakurugenzi imetangaza uamuzi wa kununua kilo milioni 30 za tumbaku kutoka kilo milioni 14 ambazo walinunua msimu uliopita. Hii ni fursa kubwa kwa wakulima wetu kwani kiasi hicho ni zaidi ya uzalishaji wa zao la tumbaku Tanzania,” amesema.

 

“Miaka ya nyuma makampuni yaliyokuwa yakinunua tumbaku yalizoea kuwapangia wakulima wetu idadi ya kilo za kununua, kwa hiyo hata uzalishaji haukuwa mkubwa sana. Nikiwa ziarani Tabora, nilikutana na viongozi wakuu wa vyama vya wakulima wa zao hili, na waliomba kupewa fursa ya kuongeza soko, kwa hiyo wakulima sasa waongeze uzalishaji ili tufikie lengo hili,” amesisitiza.

 

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya JTI, Bw. Mutsuo Iwai na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Bw. Takashi Araki.

 

Waziri Mkuu yuko Japan akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya Waziri Mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Bw. Shinzo Abe yanayotarajia kufanyika kesho.

 

(mwisho)

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATATU, SEPTEMBA 26, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.