Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kuna umuhimu wa kufikiria njia
muafaka na mbadala za kuendesha biashara
ya utalii nchini, ili kujikwamua kwa haraka, kutoka pahala ulipo sasa na kuweza kupiga hatua zaidi.
Mhe. Othman ameyasema hayo huko
hoteli ya Park Hayat mjini Zanzibar alipohutubia katika ufunguzi wa Kongamano
la kuazimisha siku ya Utalii Duniani inayofanyika kila tarehe 27 Septemba ya
kila mwaka.
Amefahamisha kwamba kufanya hivyo ni kwenda sambamba na maudhui ya
kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya Utalii mwaka huu unaosema na kuhimiza kufikiria upya
sekta ya Utalii ambao unakwenda na wakati ikizingatiwa kwamba utalii umepita katika
kipindi kigumu cha maradhi ya Korona duniani kote.
Amesema kwamba taarifa za kiutafiti zinaonesha
kwamba uchumi wa Zanzibar kupitia sekta
ya Utalii unachangia asilimia 29.2 ya
Pato la Taifa kwa Zanzibar, ambazo hazifikiwi na sekta nyengine yoyote ya uzalishaji
hapa nchini.
Aidha amesema kwamba utalii, ni
Sekta mtambuka inayotegemeana au kutegemewa na sekta nyengine zote nchini,
zikiwemo za ajira, miundombinu, nishati, uchumi wa buluu, na kilimo, na hata
upatikanaji wa huduma za kijamii na kwamba kuna ulazima kwa sekta zote
kujumuika pamoja katika kuendeleza utalii ili uimarike zaidi.
Mhe. Othman amesema kwa muda sasa,
Zanzibar imekuwa ikitegemea zaidi utalii
wa mahoteli, bahari na fukwe, na kuacha kutumia bidhaa nyingi za kitalii
zilizopo Unguja na Pemba.
Hata hivyo, Mhe. Othman amesema
umefika wakati kwa Zanzibar kuacha
kujitangaza kama ni kituo cha utalii cha Jua, Mchanga na Bahari pekee, bali itumie
pia vivutio vya kiutamaduni, historia, vyakula, dini, na matibabu , ambavyo
vinajipambanua na nchi nyengine kwa vile havipatikani popote duniani isipokuwa
Zanzibar.
Mhe. Makamu amesema kongamano hilo litachangia, kwa kiasi
kikubwa, kuuamsha ‘ulimwengu wa kitalii’ kwamba Zanzibar iko tayari kuwapokea
watalii, muda wowote , sambamba na kutekeleza itifaki ya Kudhibiti Maambukizi
ya KORONA Zanzibar kwa mashirikiano
baina ya Sekta binafsi na Serikali.
Hata hivyo Mhe. Othman ametoa wito kwamba, Kongamano hilo litumike kuleta hamasa kwa wananchi wa
Zanzibar kushiriki katika utalii ili kunufaika nao, badala ya kuendelea kubakia
kuwa mashahidi wa utalii.
Aidha, amewashajiisha wawekezaji wa
Sekta ya Utalii, kutoa kipaumbele kwa wananchi wa Zanzibar, katika ajira na
fursa nyenginezo za kiuchumi na kimaendeleo, kupitia makampuni na mashirika
wanayoyasimamia.
Naye waziri wa Utalii na Mambo ya
Kale Mhe. Simai Mohammed Said amesema
kwamba kwa kushirikiana na wadau mbali mbali
wa utalii wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza
sekta ya Utalii Zanzibar ili ulete tija zaidi kwa taifa.
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo cha Habari leo tarehe 27.09.22.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Massoud Othman akizungunza katika ufunguzi wa Kongamano la Maazimisho ya Siku ya Utalii duniani huko hoteli ya Park Hayati shangani Mjini Zanzibar .
Washiriki wa Kongamano la maazimisho ya Siku ya Utalii duniani hapa Zanzibar linalofanyika katika hoteli ya Park Hayat Shangani Zanzibar wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mhe. Othman Masoud Othman ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Kongamano hilo
No comments:
Post a Comment