Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na ujumbe wa Taasisi ya Iyilik Dernegi Kutoka Uturuki

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Viongozi wa Taasisi ya Iyilik Dernegi kutoka Nchini Uturuki, ukiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Bw.Metin Calbay.(kulia kwa Rais)  mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 3-9-2022

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Taasisi ya Iyilik dernegi kutoka nchini Uturuki kwa azma yake  ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha kuandaa utekelezaji wa miradi yote kwa nchi za Afrika Mashariki.

Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na ujumbe wa Taasisi ya Iyilik dernegi kutoka Uturuki , ulioongozwa na Kaimu Mwenyekiti wake Metin Calbay, ambapo pamoja na mambo mengine ulielezea juu ya shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo katika nchi mbali mbali Barani Afrika na Mashariki ya Kati.

Amesema amefurahishwa na azma ya Taasisi hiyo ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu kwa miradi yote inayotekelezwa na taasisi hiyo kwa nchi za Afrika Mashariki, hivyo akasema Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kufanikisha azma hiyo.

Alisema Serikali imepokea ombi la taasisi hiyo la kupatiwa eneo la Ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho  kitakachohusisha majengo ya skuli kuanzia ngazi ya maandalizi (Nursery) hadi Sekondari, chuo cha kilimo pamoja na chuo ch a ufundi.

Alieleza kufurahishwa kwake  na  misaada mbali mbali inayotolewa na taasisi hiyo kwa jamii ya Wazanzibari na kote Barani Afrika, kwa kutambua kuwa jukumu hilo ni kazi ya Serikali.

“Hii ni kazi ya serikali, lakini inapotokea taasisi ikasaidia wananchi .......tunashukuru sana”, alisema.

Katika hatua nyengine, Rais Dk. Mwinyi alishukuru na kupokea salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Kaka yake, kilichotokea hivi karibuni.

Mapema, Kaimu Mwenyekiti wa taasisi ya Iyilik dernegi, Metin Calbay alisema taasisi hiyo ina azma ya kujenga kituo kikuu hapa nchini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kudumu katika nchi za Afrika Mashariki na hivyo akaiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kupatiwa eneo  hilo ili kufanikisha jambo hilo.

Alisema ujenzi wa kituo hicho utahusisha majengo ya skuli kuanzia ngazi ya maandalizi (nursery) hadi elimu ya Sekondari, chuo cha kilimo, chuo cha ufundi na kubainisha kuwa mradi huo utaanza mara tu pale eneo hilo litakapopatikana.

Kaimu Mwenyekiti huyo alimueleza Rais Dk. Mwinyi kuwa taaisisi hiyo tayari imewasaidia wananchi wa Zanzibar Mbuzi 450 wa Maziwa pamoja na kusaidia  Mbuzi 1550 kwa ajili ya  wananchi wa Tanzania Bara, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha kiuchumi.

Metin alisema Taasisi ya Iyilik dernegi yenye makao makuu yake nchini Uturuki inajishughulisha na utoaji wa misaada katika nchi mbali mbali Barani Afrika, ikiwemo ya kugawa vyakula katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alisema taasisi hiyo pia hutoa misaada katika uchimbaji wa Visima pamoja na kutoa misaada katika maeneo yanayokumbwa na majanga, ikiwemo vita.

Alisema taasisi hiyo imefanikisha ujenzi wa nyumba na skuli kwa wakimbizi walioko katika maeneo yenye vita nchini Syria pamoja na kusaidia mbuzi Milioni tatu wa maziwa kwa nchi 25 Barani Afrika, ikiwa ni hatua  kusaidia familia zenye maisha duni.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi ya Iyilik Dernegi kutoka Nchini Uturuki Bw. Metin Calbay , alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 3-9-2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuagana na Ujumbe wa Taasisi ya Iyilik Dernegi kutoka Nchini Uturuki ukiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Bw.Metin Calbay, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 3-9-2022
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Taasisi ya Iyilik Dernegi kutoka Nchini Uturuki ukiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Bw. Metin Calbay (kulia kwa Rais) baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 3-9-2022
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.