Habari za Punde

Kamati ya Mwaka Kogwa Makunduchi Wakabidhi Msaada wa Vyakula kwa Wanafuzi Wanaojiandaa na Mitihani Kidatu cha Nne na Kukabidhi Vifaa vya Usafi Hospitali ya Wilaya Makunduchi Unguja

 

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Mhe.Rajab Yussuf Mkasaba akikabidhi Vifaa kwa ajili ya usafi kwa Hospitali ya Wilaya Makunduchi pamoja na risiti ya kielektroniki ya mafuta kwa ajili ya gari ya wagonjwa ya hospitali hiyo ambayo itawasaidia wagonjwa wanaopata rufaa ya kutoka hospitalini hapo na kwenda hospitali Kuu ya rufaa ya Mnazi Mmoja.
Mkuu wa Wilaya ya Kusini Rajab Yussuf Mkasaba aliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akipokea msaada wa vyakula kwa kambi za wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya Kidato cha Nne katika skuli ya Sekondari ya Manduchi na skuli ya Sekondari Kusini, msaada uliotolewa na Kamati ya Mwaka Kogwa ya Makunduchi.

UONGOZI wa Wilaya ya Kusini kwa kushirikiana na Kamati ya Mwaka Kogwa wameitaka jamii pamoja na wadau mbali mbali nchini kutoa misada kwa wanafunzi waliokwenye kambi za matayarisho ya mitihani ili azma ya kuimarisha sekta ya elimu na kuleta ufaulu mzuri katika Wilaya hiyo iweze kufikiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kusini Rajab Yussuf Mkasaba aliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akipokea msaada wa vyakula kwa kambi za wanafunzi wanaojiandaa na mitihani ya Kidato cha Nne katika skuli ya Sekondari ya Manduchi na skuli ya Sekondari Kusini, msaada uliotolewa na Kamati ya Mwaka Kogwa ya Makunduchi.

Katika maelezo yake Mkuu huyo wa Wilaya ya Kusini alisema kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa mikakati itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo la Serikali katika kutokomeza ufaulu mbaya wa matokeo a Kitado cha Nne katika Mkoa huo na kusaidia katika kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu.

Aidha, Mkasaba alisema kuwa Kamati ya Mwaka Kogwa imeonesha mfano mzuri kwa kugeuza changamoto kuifanya kuwa fursa baada ya kuyaona matokeo ya mitihani hayaridhishi katika Wilaya hiyo na kuweza kutoa msaada huo hatua ambayo kwa mashirikiano ya pamoja itasaidia kuleta matokea chanya.

Hivyo, Mkuu wa Mkoa huo aliipongeza Kamati hiyo kwa hatua yake hiyo na kuwaomba wadau wengine wa ndani na nje ya Makunduchi kutoa misaada yao ya hali na mali kwa wanafunzi hao ili waweze kusoma vizuri na kujiwekea maandalizi mazuri ya mitihani yao ijayo.

Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa Wilaya aligawa vifaa mbali mbali vya usafi katika Hospitali ya Wilaya ya Makunduchi pamoja na risiti ya kielektroniki ya mafuta kwa ajili ya gari ya wagonjwa ya hospitali hiyo ambayo itawasaidia wagonjwa wanaopata rufaa ya kutoka hospitalini hapo na kwenda hospitali Kuu ya rufaa ya Mnazi Mmoja.

Mkasaba alieleza kwamba misaada kama hiyo inahitajika kwa ajili ya kuisaidia jamii sambamba na kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kufikia malengo iliyoyakusudia.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Mwaka Kongwa Mzee Mwita Masemo alieleza  kwamba Kamati yake imeamua kutoa msaada kwa jamii kwa kutambua kwamba jamii ina haki ya kurejeshewa kile kilichopatikana katika sherehe hizo.

Mwenyekiti huyo aliitaka jamii kuondoa dhana potofu ya kwamba Kamati hiyo imekuwa ikipata fedha na kuzitumia pasipo kuifikiria jamii.

Nao walimu Wakuu pamoja na wanafunzi wa skuli hizo ambazo zimo katika Jimbo la Makunduchi waliahidi kuutumia vyema msaada huo na kufanya vizuri katika mitihani yao huku wakitoa shukurani zao za dhati kwa Kamati ya Mwaka Kogwa kwa msaada wao huo ambao wameupata wakati muwafaka.

Nae daktari dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Makunduchi Mohammed Mtumbwa Mnyimbi alitoa pongezi kwa Kamati hiyo kwa msaada huo wa vifaa vya usafi walioutoa ambao alikiri kwamba ni muhimu katika kukinga maradhi katika jamii kwa kutambua kwamba kinga ni bora kuliko Tiba.

Mapema uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wa Wilaya ya Kusini ulitoa shukurani kwa Kamati hiyo ya mwaka Kogwa na kutumia fursa hiyo kuwanasihi wanafunzi kusoma kwa bidii ili kuleta matokeo mazuri ya mitihani yao ijayo.

Sambamba na hayo, uongozi huo waliwataka wanafunzi wa skuli hizo kuachana na vitendo vyote ambavyo viko kinyume na maadili na pia vimekuwa vikipelekea kupunguza ufaulu wa wanafunzi.

Wakati huo huo, uongozi huo wa CCM wa Wilaya ya Kusini uliahidi kuwahimiza viongozi wa Majimbo katika Wilaya hiyo wakiwemo Wabunge na Wawakilishi kuunga mkono juhudi hizo kwa kutoa misaada yao kwa wanafunzi hao walioko katika kambi za maadalizi ya mitihani pamoja na kuisaidia hospitali ya Wilaya ya Makunduchi.   

Imetayarishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini,

Mkoa wa Kusini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.