Habari za Punde

Masheha wa Wilaya ya Kusini kuzidi kutoa elimu kwa wananchi wao juu ya kufuata Sheria na misingi ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora -DC Mkasaba

Na.Mwandishi Wetu Kusini Unguja. 

MKUU wa Wilaya ya Kusini Mhe.Rajab Yussuf Mkasaba amewahimiza Masheha wa Wilaya ya Kusini kuzidi kutoa elimu kwa wananchi wao juu ya kufuata Sheria na misingi ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora kwa azma ya kuwawezesha kutekeleza vyema majukumu yao.

Mkasaba ameyasema hayo katika ufunguzi wa Mafunzo ya siku moja ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora yaliyowashirikisha Masheha wa Wilaya hiyo ambayo yalitayarishwa na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Kusini, Kitogani.

Katika maelezo yake Mkuu huyo wa Wilaya aliwasisitiza Masheha kuhakikisha wanapokea vyama mafunzo hayo ili hatimae wakayafanyie kazi katika jamii na kuwa Mabalozi juu ya utekelezaji wa mafunzo hayo.

Alisema kuwa bado kuna baadhi ya wananchi katika jamii hawajapata uelewa juu ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora hivyo, elimu hiyo itasaidia  kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lililokusudiwa na Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora la kuiwezesha jamii kuwa na ueleza juu ya dhana hiyo.

Aliongeza kuwa dhana ya Utawala Bora ikitekelezwa huleta faida kadhaa ikiwemo matumizi mazuri ya rasilimali za nchi, maendeleo endelevu, kupungua kwa umasikini, ujinga na madhadhi, kutokomea kwa rushwa, kuimarika kwa huduma bora za jamii, kuimarika kwa amani na utulivu, kuheshimiwa kwa haki za binaadamu, utatuzi wa migogoro pamoja na kuleta ustawi wa wananchi.

Aidha, Mkuu wa Wilaya hiyo alieleza kwamba miongoni mwa vyanzo vya Haki za Binaadamu nchini Tanzania ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 amba pia, vipo vyanzo vingine vya haki za binaadamu nchini kama vile Sheria mbali mbali zilizopo.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa Utawala Bora na Haki za Binaadamu ni mambo yanayokwenda kwa pamoja hiyo ni kutokana na ukweli kwamba ukiukwaji wa misingi ya utawala bora unasababisha uvunjaji wa haki za binaadamu na uzingatiaji wa misingi ya utawala bora unasaidia ulinzi na hifadhi ya haki za binadamu.

Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zamzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi imeendelea kutekeleza wajibu wa kulinda haki za binaadamu na watu wake wka kutekeleza Sheria, Sera, Mipango, Mikakati na programu zinazotafsiri upatikanaji wa haki za mbali mbali.

Sambamba na hayo, utayari wa Serikali kwa kuwa na chombo kama Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora kinachopima na kuishauri Serikali kwenye utendaji kazi wa kulinda na kukuza haki za binaadamu ambapo ni ushahidi kuwa Tanzania ni nchi inayothamini demokrasia na kuwa ina Serikali inayowajibika vyema kwa wananchi.

“Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi na Awamu ya Sita ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan hali ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora zimeimarika na Tume imetekeleza vyema majukumu yake kwa uhuru”,alisema Mkasaba.

Nae Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Juma Msafiri Karibona alisema kuwa wananchi wanapaswa kujua Haki za Binaadamu na Utawala Bora kupitia kwa Masheha  ili waweze kutambua wajibu wao katika harakati zao za kimaisha.

Alieza kwamba Tume ya Haki za binaadamu na Utawala Bora ni Tume huru ambayo ni ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo, wananchi wanapaswa kuielewa na kutokuwa na hofu kutoa maelezo yao pale wanapopatwa na matatizo katika kijamii sambamba na kuzijua haki zao za msingi.

Imetayarishwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini,

Mkoa wa Kusini Unguja.

29.10.2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.