Habari za Punde

Mfumo Wetu wa Kodi Unahitaji Mageuzi --- Mhe. Othman

 

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman , akizungumza na Kamshina wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Nd. Yussuph Juma Mwenda (kulia kwa Makamu), aliyefika Ofisini kwa Makamu Migombani Zanzibar, Kujitambulisha na kubadilishana mawazo kuhusu mambo mbali mbali ya Maendeleo. Kulia kwa Kamshina ni Afisa wa Kitengo cha Uhusiano ZRB ndugu Makame Khamis Mohammed

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman , akizungumza na Kamshina wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Nd. Yussuph Juma Mwenda (kulia kwa Makamu), aliyefika Ofisini kwa Makamu Migombani Zanzibar, Kujitambulisha na kubadilishana mawazo kuhusu mambo mbali mbali ya Maendeleo. Kulia kwa Kamshina ni Afisa wa Kitengo cha Uhusiano ZRB ndugu Makame Khamis Mohammed

                              (Picha na Ofisi ya Makamu wa Kwanza Kitengo cha Habari)

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kunahitajika mageuzi katika Mifumo ya Ulipaji wa Kodi hapa Visiwani, ili kufanikisha matarajio ya pande zote, kwaajili ya kukwamua na kukuza uchumi wa Nchi.

Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo, akizungumza na Kamishna wa Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB), Bw.Yussuph Juma Mwenda, aliyefika ofisini kwake Migombani Jijini Zanzibar kwa lengo la kubadilishana mawazo kuhusu mambo mbali mbali yanayohusu maendeleo ya Nchi.

Amesema kuwa ukusanyaji wa kodi ni jambo muhimu katika kujenga uchumi wa Nchi, na hivyo mageuzi hayo yataleta tija iwapo yatagusa vipengele mbali mbali vinavyoizunguka ZRB, ambavyo ni pamoja na Sera, Utafiti wa Makusanyo ya Ndani, Mabadiliko ya Sheria, Mfumo wa Malipo ya Stempu, na Mzigo wa Mrundikano wa Kodi zinazofanana kwa wafanyabiashara wa Zanzibar na Wananchi.

Aidha, Mheshimiwa Othman amezungumzia haja ya Mifumo ya sasa ya Ukusanyaji wa Kodi, Bima, sambamba na Uendeshaji wa Mabenki kupitia Misingi ya Dini ya Kiislamu, akitolea mifano ya Mataifa mbali mbali yaliyofanikiwa katika kukuza uchumi wake kwa kufuata taratibu hizo, yakiwemo Malaysia na Mouritius.

Aidha, Mheshimiwa Othman, ameahidi kuipa mashirikiano ya dhati taasisi hiyo, sambamba na mashauri mbali mbali ya sera na sheria, ili kujenga ufanisi zaidi, na kwa maslahi ya maendeleo ya Nchi.

Kwa upande wake, Kamishna wa ZRB, Bw. Yussuph Mwenda, amesema matarajio makubwa ya ukusanyaji wa kodi hapa visiwani yataweza kufanikiwa, pindipo Bodi yake itapata uungwaji-mkono kutoka kwa Viongozi, Mamlaka mbali mbali zinazotawala, na pia wananchi kwa ujumla.

Akigusia juu ya mzigo wa ulipaji-kodi zinazojirudia kwa wafanyabiashara na wananchi wa Zanzibar, Kamishna Mwenda amesema kumekuwepo na maongezi pamoja na mahusiano mazuri, kati yao na Mamlaka-wenza kutoka Tanzania Bara, ili kuhakikisha kunakuwepo unafuu na hatimaye kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Katika Ujumbe wake, Kamishna Mwenda ameambatana na Maafisa mbali mbali wa Bodi yake, akiwemo Afisa kutoka Kitengo cha Mahusiano cha ZRB, Bw. Makame Khamis Mohamed.

Kitengo cha Habari 

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar

Oktoba 17, 2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.