Habari za Punde

Michuano ya Shimiwi Mkoani Tanga Kati ya Timu ya Ofisi ya Rais Ikulu na Kombaini ya Viongozi wa Shimiwi

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul akimiliki mpira wakati wa mechi ya ufunguzi kati ya timu ya Ofisi ya Rais Ikulu ambao wameifunga kombaini ya viongozi wa SHIMIWI uliochezwa Oktoba 5, 2022 katika Uwanja wa Bandari jijini Tanga.

 Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Sluhu Hassan kwa kuridhia kufanyika mchezo ya Shirikisho la Michezo ya Wiraza na Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI) kwa miaka miwili mfululizo.

Naibu Waziri Mhe. Gekul ametoa kauli hiyo Oktoba 5, 2022 wakati wa ufunguzi wa michezo ya 36 ya SHIMIWI ya mwaka 2022 yanayofanyika jijini Tanga.

“Mhe. Rais imempendeza kwamba arejeshe michezo hii mwaka jana, na sasa ni mara ya pili tunafanya michezo hii, lakini siyo michezo tu ya SHIMIWI, Mhe. Rais katika uongozi wake amerudisha michezo katika sekta zote, ameturudishia michezo ya SHIMUTA, michezo ya Baraza la Michezo ya Majeshi (BAMATA), UMISSETA, UMITASHUMTA na michezo ya UMISAVUTA ambayo ni michezo ya Vyuo vya Ualimu Tanzania” amesema Naibu Waziri Mhe. Gekul.

Aidha, Naibu Waziri Mhe. Gekul amewataka wanamichezo wa SHIMIWI kuendesha michezo hiyo kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa kuwa michezo ni udugu, mshikamano, ni afya na michezo ni ajira kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Michezo nchini ya mwaka 1995 na Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Na. 12 ya mwaka 1967 kati ya malengo ya Sera hiyo ni kuhamasisha umma kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo na michezo ya SHIMIWI ni utekelezaji wa sera hiyo ya michezo nchini.

“Natoa rai kwa viongozi wa mikoa, Mkatibu Tawala wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Wilaya na Maafisa Michezo kote nchini, tutakapomaliza michezo hii hapa Tanga, tuhakikishe tunaendeleza michezo katika maeneo yenu, ni matumaini yangu michezo hii ya SHIMIWI itakapomalizika hapa vipavi vingi vitakuwa vimeibuliwa na vitaendelezwa kwa kuwa katika mashindano haya wapo vijana ambao wanaweza kucheza katika timu zetu za taifa” amesema Naibu Waziri Mhe. Gekul.

Naibu Waziri Mhe. Gekul ameongeza kuwa michezo ni taaaluma ambayo inahitaji nidhamu ya hali ya juu na weledi kama ilivyo kwa taaluma nyingine na kusisistiza michezo ya SHIMIWI ni chachu ya upendo, mshikamano, Amani na umoja kwa watumishi wote na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.