Waziri wa Katiba na Sheria,
Mhe Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) akizungumza na Mawakili wa
Serikali (hawapo pichani) wakati akifunga mkutano wa chama Mawakili hao
kilichofanyika jijini Dodoma.
Mawakili wa Serikali
wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
Kigoma, Bw. Allan Shija (aliyeketi mbele katikati) wakifuatilia kwa makini
Hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (hayupo pichani) wakati
akifunga mkutano wa chama cha Mawakili wa Serikali uliofanyika jijini Dodoma.
Wakurugenzi Wasaidizi wa
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (hayupo pichani) wakati akizungumza na
Mawakili wa Serikali kabla ya kufunga Mkutano wa Chama cha Mawakili wa Serikali
uliofanyika Jijini Dodoma.
Na Mwandishi
Wetu, OWMS, Dodoma
Serikali yawapa Mawakili Wafawidhi wa Serikali siku
kumi nne kuanzia leo kuwasilisha orodha ya kesi zilizopo kwenye taasisi za umma
wanazofanyia kazi pamoja na majina na vyeo vya wahusika waliosababisha kesi
hizo
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akifunga Mkutano wa Mawakili wa Serikali
uliofanyika kwa siku tatu mkoani Dodoma.
Waziri Dkt. Ndumbaro amewataka Mawakili hao kuandaa
orodha ya kesi zote za madai zilizo kwenye taasisi zao; chanzo na sababu ya kesi
hizo; taarifa hiyo ieleze gharama au hasara ambayo Serikali inaweza ikaingia; na
taarifa iseme ni nani amesababisha kesi hiyo kwa jina na cheo chake; na taarifa
hizo za kesi ziwasilishwe kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya kipindi cha
wiki mbili
“Niwaelekeze Mawakili muwasilishe taarifa hizo za kesi
zilizopo kwa kuwa taasisi nyingine zimekuwa ni vyanzo vya kuzalisha migogoro na
mhusika aliyehusika kuzalisha mgogoro huo hausiki tena wala kutoa ushirikiano
kwa Mawakili kwa kuwapatia taarifa za kutosha kuendesha majadiliano, mashauri, usuluhushi
pamoja na kuiwakilisha Serikali mahakamani,” amesema Waziri Dkt. Ndumbaro
Pia, amewaeleza Mawakili wote wa Serikali wajiandae
kuelimisha umma kuhusu Katiba tuliyonayo na haki za binadamu ili kujenga uelewa
kwa wananchi na kupata hoja zao badala ya kupata hoja kutoka kwa wanasiasa
pekee hasa tunapoelekea kuwa na katiba mpya ikizingatiwa kuwa haya ni maelekezo
ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi, Chama Tawala
kinachoongoza Serikali ya Awamu ya Sita iliyopo madarakani chini ya uongozi wa
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwajengea uwezo
Mawakili wake ili wawe na ujuzi na ueledi katika masuala ya mikataba; uchumi wa
bluu; haki za binadamu; na uendeshaji wa mashtaka ili kuweza kuendesha kesi kwa
weledi na amewaasa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu; maadili; mila,
desturi na tamaduni za nchi yetu; misingi ya katiba na sheria za nchi
Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt.
Eliezer Feleshi amewaasa viongozi wa mpito walioteuliwa kuongoza Chama cha
Mawakili wa Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa kuhakikisha kuwa wanalinda
imani ya viongozi wa taasisi zao na imani ya wanachama kwa kuongoza chama hicho
kwa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wake badala ya kuwa jukwaa la siasa kwa
kuwa Serikali inategemea kupata maoni na ushauri wa kitaalam kutoka kwa
wanachama kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu taifa letu
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Katibu Mkuu
wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo amesema kuwa Wizara yake
imeyapokea maelekezo ya Mhe. Rais Samia na watayafanyia kazi ili kuratibu
utekelezaji wa majukumu ya Mawakili hao ndani ya utumishi wa umma pamoja na
kulea Chama cha Mawakili wa Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali
No comments:
Post a Comment