Habari za Punde

DC Moyo Awapongeza Chama cha Walimu Tanzania Manispaa ya Iringa kwa Kutoa Elimu Bora kwa Wanafunzi

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Mohamed Hassan Moyo akiongea na walimu viongozi wakati wa mkutano wa wa chama cha walimu Manispaa ya Iringa (CWT) na kuwapongeza kwa kazi nzuri ya kufaulisha wanafunzi kwa asilimia kubwa

Na Fredy Mgunda, Iringa.

Mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo amewapongeza walimu wa Manispaa ya Iringa kwa kuendelea kutoa elimu bora kwa wanafunzi wanaosoma katika shule hizo.

Akizungumza kwenye mkutano wa kikatiba wa chama cha walima Manispaa ya Iringa,Moyo alisema kuwa walimu wanaofundisha shule mbalimbali zilizopo Manispaa ya Iringa wamekuwa wakifaulisha wanafunzi kwa wastani unaotakiwa kitaifa.

Moyo alisema kuwa bila walimu kujituma na kujitoa kwa moyo wa dhati wanafunzi hawawezi kupata elimu bora wala hawawezi kufaulu kwa alama kubwa za kitaifa.

Alisema kuwa anatambua kunachangamoto nyingi za walimu na kuwaomba kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo kwa awamu kama ambavyo wameanza kwenye ujenzi wa madarasa,kupandisha madaraja na mishahara.

Moyo alisema kuwa suala la kikokoto amelichukua na atalifikisha sehemu husika kwa sababu lipo kitaifa zaidi hivyo aliwatoa hofu kuwa serikali inatambua changamoto ya kikokotoo.

Moyo alimazia kwa kuwataka walimu kuwa na nidhamu ya kazi kwa kuacha kunywa pombe wawapo kazini,mapenzi na wanafunzi pamoja na utolo muda wa kazi kwa baadhi ya walimu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa chama cha walimu Manispaa ya Iringa, mwalimu Frank Lupeke alisema kuwa walimu wa Manispaa ya Iringa licha ya kufaulisha kwa asilimia kubwa lakini wanakumbana na changamoto ya ubovu na uchakavu wa miundombini ya madarasa na baadhi ya nyumba za walimu ambazo zipo.

Mwalimu Lupeke alisema kuwa asilimia kubwa ya walimu wanakaa mbali na eneo la kazi kutokana kukosekana kwa nyumba za kuishi walimu na kusababisha kupunguza ufanisi wa kazi kwa walimu hao.

Alisema kuwa serikali ikifanikiwa kutatua changamoto hiyo ya miundombini madarasa na nyumba za walimu hata ufaulu na ufanisi wa kazi kwa walimu utaongezeka kwa asilimia kubwa.

Mwalimu Lupeke alimuomba mkuu wa wilaya ya Iringa Mohamed Hassan Moyo kupeleka kilio cha walimu cha kutaka kurejeshewa posho za kufundishia kama ilivyokuwa awali kwani kufanya hivyo kutarudiaha na kuongeza morali ya walimu kufundisha.

Lakini mwalimu Frank Lupeke alisema kuwa anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwapunguzia adha wananchi ya ujenzi wa madarasa kwa kuamua kujenga vyumba vya madarasa na ofisi za walimu katika kila shule sekondari nchi nzima.

Mwalimu Lupeke alimazia kwa kuwataka walimu wa Manispaa ya Iringa kuwa na nidhamu ya kazi ili kuilinda taaluma hiyo ya ualimu ambayo imekuwa ikiheshimika hata nchini na nje ya nchi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Manispaa ya Iringa (CWT) Bw.Frank Lupeke akiongea na waalimu viongozi wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho Manispaa ya Iringa
Katibu wa chama cha walimu Manispaa ya Iringa akiongea na walimu viongozi wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho.
Baadhi ya walimu viongozi wakiwa kwenye mkutano mkuu wa Chama cha walimu Manispaa ya Iringa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.